Skip to main content




FASIHI KWA UJUMLA
NADHARIA YA FASIHI

SANAA
Sanaa ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifu umbo ambalo msanii hulitumia katika kufikishia ujumbe aliokusudia kwa jamii / hadhira.
AINA ZA SANAA
a) Sanaa za ghibu (muziki)
Inategemea na matumizi ya ala za muziki (vifaa, sauti) uzuri wa umbo la sanaa ya muziki upo katika kusikia. Sanaa hii hailazimishi fanani (msanii) na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja. Mtunzi hufanya kazi kwa wakati wake na hadhira husikiliza kwa wakati wake.
b) Sanaa za ufundi
Sanaa hizi hutokana na kazi za mikono. (Mfano: uchoraji, ususi, ufinyanzi, uchongaji, uhunzi, utalizi/udalizi n.k.)
Mfano; - uchoraji hutegemea sana kuwepo kwa kalamu, karatasi, kitambaa, brashi, rangi n.k. uchongaji huhitaji mundu, gogo, tupa, n.k. Uzuri wa umbo na sanaa za ufundi upo katika kuona. Sanaa hii hailazimishi fanani na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja.
c) Sanaa za maonesho
Ni kazi mbalimbali za Sanaa ambazo hutegemea utendaji (mfano: ngoma, maigizo, majigambo, matambiko n.k) sanaa zilizomo kwenye kundi la sanaa za maonesho ni lazima ziwe na sifa zifuatazo:-
-Fanani
-Dhana inayotendeka
-Hadhira
-Mandhari
Sanaa za maonesho zinalazimisha fanani na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja, kwani uzuri wa umbo la sanaa hii upo katika kuona utendaji.
a) Fasihi
Sanaa hii inategemea ufundi wa matumizi ya lugha. Msanii ni lazima awe na uwezo wa kutumia vionjo vyote vya lugha (mfano; methali, misemo, tamathali za semi, nahau, vitendawili n.k)
Fasihi ni sanaa inayotumia lugha kufikisha ujumbe unaokusudiwa kwa hadhira inayokusudiwa. Sanaa hii pia hailazimishi fanani na hadhira kuwa pamoja, mahali pamoja.
KIELELEZO CHA SANAA


Kila kipengele cha Sanaa kinatofautiana na kingine kwa umbo na matumizi. Fasihi ni kipengele cha sanaa kinachotumia maneno kuumba huo uzuri wa kisanaa
TOFAUTI KATI YA FASIHI NA TANZU ZINGINE ZA SANAA
i. LUGHA
Kazi zote za fasihi zinaundwa kisanaa kwa kutumia lugha inayotamkika na inayoandikika ambayo hubeba ujumbe fulani tofauti na sanaa zingine kama vile.
- Ufinyanzi hutumia udongo
- Uchoraji hutumia kalamu, rangi, karatasi au kipande cha nguo.


ii. WAHUSIKA
Kazi ya fasihi hulazimika kuwa na wahusika wake ambao matukio mbalimbali yanayohusu jamii inayowazungukia. Hutumika kutoa dhamira ya mwandishi, Pia hutumiwa kuwasilisha tabia za watu waliomo ndani ya jamii
iii. MANDHARI
Fasihi huwa na mandhari ambayo huonyesha tukio linapofanyika. Mandhari inaweza kuwa ya kubuni au ya ukweli.
iv. UTENDAJI
Utendaji hujitokeza hasa katika kazi ya fasihi simulizi ambazo hushirikisha hadhira na fanani mahali pamoja na kwa wakati mmoja, Hapa fanani huweza kuonesha matendo katika usimuliaji wake.


v. FANI NA MAUDHUI
Fasihi ina sehemu hizi mbili za fani na maudhui ambazo hutegemeana na hufungamana. Fani ni namna msanii anavyosema kuhusu kile kinachosemwa wakati maudhui ni kile kinachosemwa na msanii.
USANAA WA FASIHI
Usanaa wa fasihi hujitokeza katika vipengele vifuatavyo:
Mtindo
Sanaa katika fasihi hujidhihirisha katika namna ya kueleza jambo, Hapa kinachoangaliwa zaidi ni zile mbinu mbalimbali zinazotumiwa na msanii katika kueleza jambo husika. Jambo huweza kuelezwa katika fumbo kwa kupitia; shairi, tamthiliya, hadithi, kitendawili n.k.
Muundo
Huu ni mpangilio mzuri wa visa na matukio. Matukio katika kazi za fasihi hupangwa kiufundi ili yaweze kuwasilishwa vizuri kwa hadhira au jamii husika.
Uteuzi mzuri wa “lugha”:
Iliyojaa vionjo mbalimbali kama vile nahau, misemo, tamathali za semi, taswira na ishara. Lugha inaweza kuchekesha, kukosoa, kukejeli, kubeza, kushawishi n.k


Uundaji mazuri wa “wahusika”.
Wahusika huumbwa kulingana na nia na lengo la mwandishi kwa hadhira wake.
Ujenzi mzuri wa “Mandhari”.
Kazi ya fasihi ni lazima iwe kwenye madhari maalum. Mandhari ikijengwa vizuri husaidia sana kujenga hisia inayokusudiwa na mwandishi kwa hadhira wake ili iwezeshe pia kufiksha ujumbe mahsusi uliokusudiwa.

FASILI ZA FASIHI
FASIHI NI KIOO
Fasihi ni kioo kwa kuwa fasihi inaweza kufananishwa na kioo. Kioo katika maisha ya kawaida huweza kumuonesha binadamu mazuri aliyonayo au mapungufu aliyonayo ili aweze kujikubali au kujikataa. Hivyo fasihi pia ina uwezo wa kuonyesha mazuri au mapungufu yaliyomo ndani ya jamii, aidha kwa jamii au kwa baadhi ya vikundi vilivyomo ndani ya jamii ambavyo huweza kuwa tofauti na mahitaji ya jamii nzima.
Udhaifu:
-Udhaifu unaojitokeza katika fasihi hii ni kwamba fasihi ina uwezo wa kuonesha mambo kama ni mabaya au mazuri lakini haina uwezo wa kuonesha njia ya kutatua matatizo hayo kama kilivyo kioo.
Udhaifu wa fasili ya fasihi ni hisi
Je ni mara ngapi mwanafasihi ataguswa ndipo aweze kuandika kazi ya fasihi? Je ni mwandishi pekee ndiye anayetakiwa kuguswa? Ukweli ni kwamba sio kazi zote zinazoandikwa zinataokana na mguso unaompata mwandishi.
FASIHI NI MWAMVULI
Fasili ya fasihi ni mwamvuli ilifananishwa na mwamvuli kwa jinsi inavyoweza kumhifadhi binadamu kwa jua au mvua lakini nadharia halisi ya fasili kufananishwa na mwamvuli ni katika uelekeo wa kwamba fasihi inauwezo wa kulinda amali za jamii zisipotee na zisiweze kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
Udhaifu: - fasili hii ilionesha udhaifu wa fasihi kutokuwa na uwezo wa kulinda amali za jamii yaani mila na desturi zilizopotea kwani mila na desturi ndani ya jamii huwa zinaenda na wakati na hubadilika kulingana na mahitaji ya wakati huo.
iii. FASIHI NI HISI
Dhana hii ilikuwa na maana kwamba kazi ya fasihi inapoletwa mtoaji/ msanii ni lazima awe anaguswa na jambo fulani na ndipo aweze kuandika kazi hiyo.
FASIHI NI KIELELEZO CHA KISANAA
Fasihi inatazamwa Kama ni ubunifu au ufundi wa aina fulani unaojidhihirisha katika maandishi.
Udhaifu: - fasili hii huzingatia zaidi utoaji wa burudani tu na hauzungumzii lolote juu ya uelimshaji wa nini kifanyike juu ya tatizo alilolionesha msanii.
FASIHI
Fasihi ni sanaa inayotumia lugha ambayo msanii huitumia ili kuweza kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa. Fasihi huwa ina umbo timillifu, Mfano kazi ya fasihi inaweza kuwa tamthiliya (igizo), hadithi au ushairi.
Uhai wa lugha katika kazi ya fasihi inaongeza mvuto. Lugha inaweza kupewa uhai huo kwa kutumia tamathali za semi kama vile tashibiha, tasfida, sitiari, kejeli, dhihaka, balagha kijembe n.k. vipengele vingine vinavyotawala ufasihi ni uundaji wa wahjusika, maatumizi ya picha, mandhari, utendaji, n.k
Mfano:-
Mtoto aloumbika, mara mtoto laini
Shingo yake ya birika, watabasamu moyoni
Kweli asali tamu, wajua ilivyoundwa
Hapa unaweza kupata ujumbe kwa kupitia maswali mbalimbali.
Mhusika ameumbwaje?
Shingo yake inafananishwa na nini
Uzuri wa mototo umeoneshwaje?
Asli imetumika kwa sababu gani?
Swali lililo kwenye mstari wa mwisho limeulizwa kwa sababu gani?
MADHUMUNI YA FASIHI
Fasihi ni kazi inayotokana na jamii na ipo kwa ajili ya jamii.
Kazi ya fasihi na fasihi yenyewe huathiriwa na mazingira na maendeleo ya jamii.
MADHUMUNI
Fasihi hushughulikia mahusiano ya jamii, hivyo basi fasihi:-
Hueleza ukweli wa maisha ya jamii
Hujenga udadisi kujielewa na kuelewa watu wengine
Huendeleza, hudumisha na kurithisha utamaduni wa jamii
Huonesha jamii njia na mitindo mbalimbali ya kujieleza
Huburudisha kupitia mvuto ulimo ndani ya LUGHA, MUUNDO na MAUDHUI yake.
Huijenga jamii kifikra na kisiasa ili kuwezesha kutoa maamuzi na kuwa na msimamo wa maamuzi hayo.

DHIMA YA FASIHI
1) Huelimisha, katika kupitia maonyo (huonya) hutohamisha ukweli, huelekeza, hutoa mawaidha na kuonesha mwanga wa migogoro.
2) Huburudisha kupitia maliwazo (huliwaza), hufundisha,hubembeleza, huhamasisha, hutuliza mawazo.
DHIMA YA MWANAFASIHI
1) Huelimisha
Hufanya kazi ya kuelimisha kwa kukosoa, kutia hamasa, kuonya, kueneza mawazo na falsafa za jamii
2) Huburudisha
3) Huhifadhi na kurithisha amali za jamii.
4) Hudumisha na kuendeleza lugha


MATUMIZI YA FASIHI
Matumizi ya fasihi hutegemea sana msimamo na mikabala ya wasimulizi na waandishi. Kwa kawaida mtunzi hujiambatisha na tabaka Lake. Kwa hali hii ndiyo maana:
1) Mwandishi wa tabaka la watawala kutetea kwa kusifia tabaka hilo
2) Mwandishi wa tabaka la wakandamizwaji ataandika maudhui ya kujikomboa yaani kulikomboa tabaka lake.
3) Anayetokana na udhamini, utunzi wake hulazimishwa kutetea tabaka lisilo lake ama kwa hofu, kwa malipo au yote kwa pamoja.



UHURU WA MTUNZI WA KAZI ZA KIFASIHI
Ni hali ya mwandishi wa fasihi kuwa huru na wazi kutoa mawazo yake na hisia zake kwa jamii bila ya kupingwa na tabaka lolote.
Au ni ile hali ya kutunga au kuandika kazi yake bila kushinikizwa na mtu, watu au taasisi fulani yenye nguvu kiuchumi, kisiasa na kitawala. Mtunzi wa kazi ya fasihi anakuwa na uwezo wake binafsi wa kufanya maamuzi juu ya fani na maudhui ya kazi yake.
NGUZO KUU ZA DHANA YA UHURU WA MTUNZI WA KAZI ZA KIFASIHI
1) UTASHI
Ni hali ya kuamua kuazimia au kukusudia jambo bila kushurutishwa au kuyumbishwa.Moja ya dhima ya mtunzi ni kuiamsha jamii iweze kutambua unyonyaji, ukandamizaji na uonevu uliomo ndani ya jamii ili iweze kuchukua hatua ya kukomesha hali hizo. Hivyo mtunzi anapotimiza dhima hii anaweza kukabiliana na tabaka kandamizi. Hapo ndipo utashi wa mtunzi unapoweza kumwelekeza kusonga mbele na jukumu lake au kuwa kasuku wa kusifia tabaka tawala au kandamizi kwa kufunika maovu ya tabaka hilo au kujiondoa kabisa kwenye ulingo wa fasihi.
Mfano Ngugi wa Thiong’o aliwahi kuhukumiwa na serikali ya Kenya alipoandika tamthiliya ya “THIS TIME TOMORROW” kwa kukosoa uovu wa tabaka tawala. Utashi umemfanya mpaka leo aendelee na msimamo wake ule ule.
2) FALSAFA
Mwandishi anapaswa kuwa na falsafa moja inayoeleweka ambayo huyafanya maandishi yaonekane kama kazi moja yenye mwelekeo maalum. Mwandishi akipoteza uhuru huweza kuyumbishwa kirahisi; Mfano mwandishi anaweza kuandika kuhusu ujamaa, kesho akaandika kuhusu mapenzi, kesho kutwa kuhusu ubepari
Mwandishi asiye huru huwa ni mtumwa wa hali mbalimbali za maisha zinazomfanya ayumbeyumbe huku na kule.
3) SANAA
Mwandishi anapaswa kuwana weledi wa misingi ya aina ya utunzi wa sanaa anayotaka kuitumia kufikisha ujumbe wake. Mfano: Akitaka kufikisha ujumbe kwa njia riwaya ni lazima ajue barabara misingi ya uandishi wa riwaya vinginevyo msanii hatokuwa na uhuru wa kisinaa maana hatakuwa na namna yenye nguvu ya kukisema hicho alichonacho.
4) LUGHA

Msanii ambaye hana weledi wa lugha na misingi ya lugha anayoitumia ni lazima atajikuta amefungwa. Hatakuwa na uhuru wa kusema kile kilichomo nafsini mwake kwa ufasaha na kwa mafanikio.


DHIMA YA UHURU WA MWANDISHI
Mwandishi awe huru kuikosoa jamii au kulikosoa tabaka lolote linalokwenda kinyume na maadili ya jamii
Mwandishi awe na falsafa inayoeleweka na utashi
Kuikomboa jamii kutoka katika fikra mbovu za kugandamizwa, kunyonywa na kuonewa na tabaka tawala.
Uandishi wa kikasuku kupungua
Unaifanya fasihi kuwa chombo cha kuikomboa jamii KIUCHUMI, KISIASA, KIUTAMADUNI, KIJAMII NA KIFIKRA.
Mwandishi anakuwa na uhuru wa kuisukasuka jamii bila matatizo yoyote.
UDHAMINI
Udhamini wa kazi ya fasihi ni kitendo cha mtu au chombo fulani kukubali kufadhili au kugharamia kazi ya mtunzi ili iweze kuchapishwa na hatimaye kusambazwa mahali mbalimbali hadi iwafikie walengwa.
AINA ZA UDHAMINI
UDHAMINI WA KISHAWISHI
Huu ni udhamini ambao mdhamini humshawishi mtunzi wa kazi ya fasihi aidha kwa fedha au masilahi mengine. Hali hii humfanya mtunzi kwa hiari yake kuingia katika udhamini.
UDHAMINI WA NGUVU
Huu ni udhamini ambao hutolewa na vyombo vya dola. Mtunzi huingia katika udhamini huu kwa lazima. Dola hudhamini watunzi ili waweze kuandika kile kilichoagizwa na dola. Hivyo mtunzi huandika na kuingia katika udhamini huu kwa nguvu ya dola kwa kuogopa aidha kazi zake kuzuiwa au kuondolewa kabisa katika ulimwengu fasihi.
UDHAMINI WA MTUNZI MWENYEWE
Huu ni udhamini ambao mtunzi mwenyewe hujisimamia binafsi katika kugharamia gharama zote za uhariri, uchapaji na usambazaji wa kazi zake. Mara nyingi hufanywa na watunzi wenye uwezo
UDHAMINI WA MAKAMPUNI YA UCHAPISHAJI
Yapo makampuni mbalimbali ya uchapishaji ambayo hupokea miswaada kisha wanaithamini, wanaihariri, wanaichapisha na kuisambaza kwa wasomaji. Makampuni haya hutoa fedha kwa ajili ya mambo yote hayo kwa matarajio ya kurudisha pamoja na faida wakati wa mauzo ya kazi inayohusika.
DHIMA YA UDHAMINI WA KAZI YA FASIHI .
(a) Kuwawezesha watunzi wasiokuwa na uwezo wa kifedha kuchapisha kazi zao na kuzifikisha kwa hadhira.
(b) Kuibua vipaji vya watunzi. Kwa kawaida kuna watu wengi wenye vipaji lakini hawavitendei haki kwa vile hawana uwezo wa kuendelea na hatua za mbele kama vile uchapishaji na usambazaji.
(c) Mdhamini hujitangaza. Udhamini humuwezesha mdhamini kujitangaza ama kibiashara au kupata heshima miongoni mwa jamii.
(d) Ni njia ya kuleta kipato kwa wadhamini. Kwa mfano kwa makampuni ya uchapishaji.
(e) Kuwapatia watunzi fedha za haraka kabla na baada ya kazi kuuzwa.
(f) Kuwainua watunzi chipukizi kwa kuwawezesha kufikisha kazi zao kwa hadhira ili ujumbe uliokusudiwa uwafikie waliokusudiwa.
(g) Kuwafanya watunzi chipukizi kufahamika.


ATHARI ZA UDHAMINI WA FASIHI.
Udhamini wa kazi za fasihi una athari mbalimabali, zifuatazo ni baadhi ya athari hizo :-
(a) Mtunzi huandika kazi yake kulingana na matakwa ya mdhamini. Kwa mfano iwapo udhamini uliotolewa na kazi zilizo katika lugha ya kiingereza, msanii anayetumia lugha ya Kiswahili kuandika kazi zake hawezi kufaidika na udhamini huo.
(b) Mtunzi hushindwa kuandika mambo kulingana na mtazamo wake halisi juu ya jamii inayo mzunguka.
Mtunzi hushindwa kukosoa uovu hasa unapokuwa unamhusu mdhamini wa kazi yake.Kwa mfano serikali au tabaka tawala.
(c) Kukua kwa fasihi pendwa kwa mfano riwaya pendwa na, kudumaa kwa fasihi dhati mfano riwaya dhati. Hali hii inatokana na msukosuko wa kibiashara. Fasihi pendwa inauzwa kirahisi sokoni. kwa kuwa na maudhui yenye msisimko kwa mfano upelelezi, usambazaji, mauaji, mapenzi n.k.
(d) Mapana ya kijographia na utafiti wa fasihi kabla ya kuandikwa hutegemeana na uwezo wa kifedha wa mdhamini.
(e) Uhuru wa mwandishi hutoweka.



Popular posts from this blog

MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI FASIHI SIMULIZI: Fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutumia mazungumzo na matendo katika kuwasilisha ujumbe Fulani kwa watazamaji au wasikilizaji. Mazungumzo hayo huweza kuwa ya kuimbwa kutendwa au kuzungumzwa, Aina hii ya fasihi imepokelewa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. Msimulizi katika fasihi simulizi mbali na kutumia mdomo wake hutumia viungo vyake vya mwili kama mikono, miguu, ishara mbalimbali katika uso wake na hata kupandisha na kushusha sauti yake. Kwa ujumla anaweza kutumia mwili wake mzima katika kuwasilisha na kufanikisha ujumbe wake kwa hadhira yake ambayo huwa ana kwa ana. Isotoshe anafaulu katika kutoa picha halisi ya dhana anayotaka kuiwasilisha kama ni ya huzuni, furaha, kuchekesha n.k. Zaidi ya kusimulia, kuimba na kuigiza msanii wa fasihi simulizi huwa na nafasi ya kushirikisha hadhira yake kama wahusika katika sanaa yake. Anaweza kutimiza hayo kwa kumfanya mshiri...
MAENDELEO YA KISWAHILI ASILI YA LUGHA YA KISWAHILI Neno asili lina maana kuwa jinsi kitu au jambo lilivyotokea au lilivyoanza na tunapozungumzia asili ya lugha ya Kiswahili ina maanisha tunachunguza namna lugha hiyo ilivyoanza. Wataalamu mbalimbali wa lugha wamefanya uchunguzi juu ya asili ya lugha ya Kiswahili. Uchunguzi huo umejenga nadharia mbalimbali zinazoelezea chimbuko la lugha ya Kiswahili. Kwa ujumla historia kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili ina matatizo mengi na ndiyo maana kuna nadharia mbalimbali zinazoelezea juu ya asili ya lugha ya Kiswahili. Miongoni mwa matatizo yanayoikabili historia ya Kiswahili ni pamoja na: Hakuna uthibitisho kamili juu ya nadharia zinaelezea asili ya lugha ya Kiswahili na kuenea kwake. Uchunguzi wa asili ya Kiswahili ulifanywa na wataalamu wa kizungu ambao waliandika historia ya Kiswahili jinsi walivyoelewa wao baada ya kupata ushahidi kidogo tu. Wazawa hawakushirikishwa ipasavyo katika uchunguzi wa lugha ya Kiswahili. Hapakuwa na k...
VIAMBISHI Baadhi ya watu huchanganya dhana ya viambishi na dhana ya mofimu. Lakini ukweli ni kwamba mofimu na viambishi ni dhana mbili tofauti zenye mabwiano Fulani pia. Kwa ujumla viambishi vyote ni mofimu na mofimu zote ni viambishi SWALI: VIAMBISHI NI NINI? Viambishi ni mofimu zinazoandikwa kwenye mizizi wa neno ili kukamilisha muundo wa neno husika. Katika lugha ya Kiswahili viambishi vinaweza kuandikwa kabla ya mzizi wa neno na baada ya mzizi wa neno. kwa hiyo katika lugha ya kiswahili viambishi hutokea kabla ya mzizi wa neno na baada ya mzizi wa neno AINA ZA VIAMBISHI Lugha ya Kiswahili ina viambishi vya aina mbili VIAMBISHI AWALI/TANGULIZI Hivi ni viambishi ambavyo hutokea mwanzoni mwa mzizi wa neno na huwa ni vya aina mbalimbali A.Viambishi idadi /ngeli Viambishi hivi hupatikana mwanzoni mwa majina vivumishi kwa lengo la kuonesha idadi yaani wingi na umoja, Mfano : M – cheshi wa –zuri M – tu wa - tu Ki – ti vi-ti ...
AINA ZA SENTENSI Kuna aina kuu nne za sentensi Sentensi changamano Sentensi sahili/ huru. 3. Sentensi shurutia Sentensi Ambatano 1.SENTENSI SAHILI/HURU Hii ni aina ya sentensi ambayo hutawaliwa na kishazi huru. Kishazi hicho kinaweza kuwa kifungu tenzi kimoja ambacho kinaweza kuwa na kitenzi kikuu au kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu au kitenzi kishirikishi na shamirisho Mfano: Juma ni mzembe Juma alikuwa mzembe sana Mwalimu alikuwa nafundihsa darasani MIUNDO YA SENTENSI HURU /SAHILI Muundo wa kitenzi kikuu peke yake (tawaliwa) Mfano: Wanacheza Alinipiga Wanasoma i.Muundo wa kitenzi kikuu peke yake (tawaliwa) Mfano: Wanacheza Alinipiga Wanasoma ii.Muundo wa kitenzi na kitenzi kikuu Mfano: Alikuwa anasoma Walikuwa wanataka kufundishwa ii Muundo wa kirai na kirai kitenzi Mfano; Mwalimu anafundisha Wanafunzi wanamsikiliza iii. Muundo wa virai vite...
UTUMIZI WA LUGHA Matumizi ya lugha ni namna yakutumia lugha kulingana na mila, desturi na taratibu zilizopo katika jamii husika. Ni jinsi ambavyo mzungumzaji anatunza lugha kwa kuzingatia uhusiano wake na yule anayezungumza naye. Matumizi ya lugha hutegemea mambo kadhaa Kama vile: Uhusiano baina ya wazungumzaji. -Mada inayozungumzwa -Mazingira waliyomo wazungumzaji n.k Umuhimu wa matumizi ya lugha Kuwasaidia watumiaji wa lugha kutumia lugha kwa ufasaha Kumsadia mzungumzaji kuweza kutambua kutofautiana na kutumia mitindo mbalimbali ya lugha MTINDO WA LUGHA Mtindo wa lugha ni mabadiliko yanayojitokeza katika kutumia lugha mabadiliko ya lugha katika mitindo mbalimbali yaani mitindo mbalimbali ya lugha. Kwa kawaida mtindo wa lugha / mabadiliko katika kutumia lugha ndiyo inayomwongoza mzungumzaji katika kuelewa maneno na mitindo ya tungo, Matumizi katika lugha hutawaliwa na mambo ya...
MATUMIZI YA SARUFI NADHARIA ZA SARUFI Dhana ya sarufi ya lugha imefafanuliwa na wataalamu mbalimbali wa sarufi. Mtaalamu James Salehe Mdee (1999) sarufi ya Kiswahili sekondari na vyuo anafafanua maana ya sarufi kuwa ni mfumo wa kanuni za lugha zinazomwezesha mzungumzaji kutunga sentensi sahihi na zenye kukubaliwa na wazawa wa lugha. Kanuni hizi hujitokeza katika lugha ya mzawa wa lugha inayohusika ambaye anaifahamu barabara lugha yake. Sarufi inajumuisha mfumo wa sauti maumbo ya maneno muundo na maana. Mtaalamu Mbundo Msokile (1992) na khamisi (1978) wanasema sarufi ni mfumo wa taratibu na kanuni zinazotawala matumizi sahihi ya matamshi, maumbo ya maneno, miundo ya tungo na maanda ya miundo ya lugha. Ni mfumo wa taratibu zinazomwezesha mzungumzaji wa lugha kutoa tungo sahihi na pia inamwezesha mtu yeyote anayezungumza kuelewa tungo zinazotolewa na mtu mwingine anayetuma lugha hiyo hiyo. F. Nkwera (1978) anasema sarufi ni utaratibu wa kanuni zinazomwezesha mzawa au mtumiaji ...
NOMINO /MAJINA (N) Majina ni aina ya maneno ambayo hutaja vitu, viumbe, hali au matendo ili kuviainisha na kuvitofautisha na vitu vingine. Mfano: Winnie, Werevu, Wema, Lulu, Mtu, Ubungo, Mungu na n.k AINA ZA MAJINA a.Majina ya kawaida Majina haya yanataja viumbe kama vile wanyama, miti, watu, ndege, wadudu. Majina yote hayo yanapoandikwa huanza kwa herufi ndogo kama yanatokea katikati ya sentensi au tungo. N:B Majina hayo sio maalumu kwa vitu Fulani tu bali kwa vitu mbalimbali. b. Majina ya Pekee. Haya ni majina maalumu kwa watu au mahali ambaye huonesha upekee kwa watu,mahali au vitu, Majina haya hujumuisha majina binafsi ya watu na majina ya mahali. Mfano: Marcus, Halima, James, Abel, Fredy, Anna Ubungo, Manzese, Tanzania, Uingereza, Africa N: B Majina hayo yanapoandikwa huanza kwa herufi kubwa C. Majina ya jamii. Haya ni majina ambayo yanataja vitu au watu wakiwa katika makundi au mafungu japo huwa majina hayo yapo katika hali ya umoja. Mfano,...
KUBAINISHA MOFIMU Kubainisha mofimu ni kuligawa neno katika mofimu zinazolijenga neno na kueleza kazi za kila mofimu ubabaishaji huo wa mofimu hufuata hatua zifuatazo 1. Kutambua aina ya neno – Yaani kama neno hilo ni tegemezi au neno changamano, Neno huru huundwa na mofimu huru na neno tegemezi huundwa na mofimu tegemezi na neno changamano huundwa na moja huru na mengine tegemezi N: B Neno huru huwa halivunjwi vunjwi kwani huundwa na mofimu huru 2. Kulitenga neno na kulivunja vunja katika mofimu zinazojenga neno hilo yaani hujenga mofimu awali, mzizi na mofimu tamati. N: B Mofimu awali, mzizi na mofimu tamati hupatikana katika maneno tegemezi na maneno changamano 3. Kueleza kazi ya kila mofimu Mfano: Bainisha mofimu katika maneno yafuatayo Hatukupendi Hili ni neno tegemezi ii. 1- Mofimu awali kianzishi, nafsi ya kwanza wingi 2 - Mofimu awali rejeshi kwa mtendwa 3 - Mofimu awali rejeshi kwa mtenda 4 - Mofimu mzizi 5 ...
UTUNGAJI Maana ya utungaji Utungaji ni pato la akili ya mtu binafsi ambayo hurejeshwa kwa fani kama vile macho, ushairi, tamthiliya au hadithi. Utungaji ni kitendo cha kuyatoa mawazo ubongoni, kuyakusanya na kisha kuyadhihirisha kwa kuyaandika au kuyazungumza. Ni kitendo cha kuunda hoja na kuyapanga katika mtiririko unaofaa katika lugha kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii husika. SIFA ZA MTUNGAJI Mtunzi analazimika kuelewa kikamilifu mada inayoshughulikiwa. Mtungaji lazima azingatie kanuni na taratibu za uandishi. Mtungaji anatakiwa kuzingatia mpango mzuri na wenye mantiki wa mawazo kutoka mwanzoni hadi mwishoni. Mtungaji anapaswa kuwa na msamiati wa kutosha ili kumwezesha kutumia lugha bora, sanifu, na fasaha. Mtunzi anapaswa kuzingatia sarufi ya lugha anayoitumia. Mtunzi anapaswa kujali nyakati zinazofaa. Mtunzi anapaswa kuwa na uwezo wa kutosha wa kuhusisha yanayoelezwa na hali halisi ilivyo katika j...