UTUNGAJI
Maana ya utungaji
Utungaji ni pato la akili ya mtu binafsi ambayo hurejeshwa kwa fani kama vile macho, ushairi, tamthiliya au hadithi. Utungaji ni kitendo cha kuyatoa mawazo ubongoni, kuyakusanya na kisha kuyadhihirisha kwa kuyaandika au kuyazungumza. Ni kitendo cha kuunda hoja na kuyapanga katika mtiririko unaofaa katika lugha kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
SIFA ZA MTUNGAJI
Mtunzi analazimika kuelewa kikamilifu mada inayoshughulikiwa.
Mtungaji lazima azingatie kanuni na taratibu za uandishi.
Mtungaji anatakiwa kuzingatia mpango mzuri na wenye mantiki wa mawazo kutoka mwanzoni hadi mwishoni.
Mtungaji anapaswa kuwa na msamiati wa kutosha ili kumwezesha kutumia lugha bora, sanifu, na fasaha.
Mtunzi anapaswa kuzingatia sarufi ya lugha anayoitumia.
Mtunzi anapaswa kujali nyakati zinazofaa.
Mtunzi anapaswa kuwa na uwezo wa kutosha wa kuhusisha yanayoelezwa na hali halisi ilivyo katika jamii kwa mifano dhahiri.
AINA ZA UTUNGAJI:-
Utungaji wa mazungumzo
Utungaji wa maandishi
UTUNGAJI WA MAZUNGUMZO
Utungaji wa mazungumzo unahusisha kujieleza kwa njia ya mdomo kwa lengo la kueleweka.
LENGO
-Hutuwezesha kujieleza kwa ufasaha katika kila fani.
-Hutuwezesha kutumia lugha inayotakiwa katika jamii.
-Hujenga moyo/hali ya kujiamini katika kuzungumza
-Kukuza kiwango cha wasikilizaji kwa makini kutoa uamuzi unaofaa.
-Kutuwezesha kutambua lugha inayofaa katika kujieleza kutokana na lafudhi, shada, matamshi na miundo.
MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA UTUNGAJI WA MAZUNGUMZO
Kusikiliza kwa makini, kuchambua na kuelewa vema mada inayozungumzwa. Kuzungumza kwa umakini na kufafanua kwa umakini mada unayozungumza, anapaswa kuzingatia mpango mzuri wa mawazo wenye mantiki kutoka mwanzo mpaka mwisho.
Mtunzi anapaswa azingatie hadhira anayozungumza nayo.
Mzungumzaji lazima awe na uwezo wa kufafanua na kuhusisha anayozungumza na hali halisi ilivyo katika jamii yetu.
Mzungumzaji anapaswa awe na msamiati wa kutosha utakaomwezesha kutumia lugha bora, kujieleza vizuri na kutunza lugha sanifu na fasaha.
Ni vizuri mzungumzaji akazingatia sarufi ya lugha anayotumia na kujali nyakati.
UTUNGAJI WA KUANDIKA
Ni uwezo wa kujieleza katika maandishi au uwezo wa kutoa mawazo binafsi na kuyaweka katika kiwakilishi cha maandishi. Utungaji wa kuandika tofauti kidogo na utungaji wa kuzungumza. Tofauti hizo hujitokeza katika kiwakilishi uwasilishaji wake.
Mazungumzo ya chanzo na kikomo na uhusiano baina ya mwandishi na msomaji. Kutokana na tofauti hizo katika utungaji wa kuandika maandishi zaidi yanahitajika ukilinganisha na utungaji wa kuzungumza.
MAMBO YA KUZINGATIWA KATIKA UTUNGAJI WA KUANDIKA
Mwandishi aelewe vema mambo anayoandika.
Mwandishi anatakiwa kuzingatia mpango mzuri wa mawazo wenye mantiki kutoka mwanzo hadi mwisho.
Mtungaji anapaswa awe na msamiati wa kutosha utakaomuwezesha kutumia lugha iliyobora, sanifu na fasaha.
Mtungaji anapaswa awe na uwezo wa kubebesha yale anayoyaeleza na hali halisi ilivyo katika jamii yetu. Ni vizuri akatoa mifano dhahiri.
Kuzingatia matumizi bora ya vituo na alama mbalimbali za uandishi kuwa na utangulizi mzuri wenye kuvutia… ya watu na hitimisho zuri.
Mtungaji anapaswa kuzingatia sarufi ya lugha anayoitumia na kujali nyakati.
Matumizi ya vituo na alama mbalimbali za uandishi:-
Alama ya mkato (,)
Alama hii hutumika kwa kazi zifuatazo:-
(a) Kuweka pumziko fupi katika sentensi.
Mfano: tulipofika nyumbani, tulikula chakula.
(b) Kutenga maneno yaliyo katika orodha.
Mfano: ukifika sokoni nunua matunda, dagaa, mkaa, unga, na sabuni ya kufulia.
(c) Kuonesha sehemu mbili za sentensi zilizo kinyume.
Mfano:- Sisi wanadamu hupanga, Mungu hupangua.
-Ulisema utakuja, hukuja
(d) Kutumiwa kabla ya alama za mtajo.
Mfano: Juma alimwambia Khadija, Nakupenda kama pipi.
(e) Kuonesha vyeo, viwili au masikani baada ya jina la mtajwa
Mfano: Philemon Ndesamburo
Mbunge wa Moshi mjini,
S.L.P 11646,
Ngangamfumuni,
2. Nukta ( . )
Alama hii hutumika kama ifuatavyo:-
(a) Hutumika kukamilisha sentensi na hivyo kuweka pumziko kubwa tunaposema.
Mfano: Mtoto wangu nampenda sana.
(b) Kuonesha ufupisho wa maneno.
Mfano: S.L.P - Sanduku la posta
n.k - nakadhalika
(c) Kuonesha vipimo mbalimbali katika desimali
Mfano: kg. 80. 3
-Saa 2.30
Nukta mkato ( ; )
Alama hii hutumika kama ifuatavyo:-
(a) Kuunganisha sentensi mbili zinazoweza kusimama zenyewe bila kutumia kiunganishi.
Mfano: Hapo zamani watu walijiheshimu sana; Siku hizi hawajiheshimu kabisa
(b) Hutumika ili kupumzika katika sentensi iliyondefu sana, kuliko unapotumika mkato.
Mfano: Alipomtazama alibaini kuwa alikuwa Malaya wa kutupwa; Hivyo aliamua kuachana naye.
Nukta mbili / pacha (:)
Alama hii hutumika kama ifuatavyo,
(a) Hutumika kutaja maneno yaliyo katika orodha.
Mfano: Niletee vitu hivi: wino, karatasi, kalamu, kiberiti, daftari, wembe, ndimu, chungwa na ndizi.
(b) Hutumika badala ya alama ya mkato.
Mfano: Alipomwona alianza kumshambulia kwa maneno:
-“Nakujua wewe huna lolote, mlevi kama wewe!”
(c) Hutumika baada ya kuandika jina la mhusika katika tamthiliya.
Mfano: Julia: Kwani hujui kuwa Nungungungu anavusha kahawa na almasi kwenda nje kwa magendo?
Mlemeta: Sijui
Julia: Hujui kuwa Nungunungu anaakaunti na hoteli Uswizi?
(d) Kutenganisha dakika na sekunde.
Mfano: Saa 8:30:48
(e) Kuonesha uwiano baina ya namba.
Mfano: Juma na Hamisi waligawana machungwa 20 kwa uwiano ufuatao: 3:7. Je, kila mmoja alipata machungwa mangapi?
Alama ya kushangaa ( ! )
Alama hii kutumika kama ifuatavyo:-
(a) Hutumika kuonesha vionjo vya moyo kama vile furaha, huzuni , chuki.
Mfano: Kumbe Juma alikuwa mwizi wa mitumba!
(b) Hutumika wakati wa kusisitiza, kubeza, kutunza n.k
Mfano: Kwenda! Mwone kwanza alivyo! Uso umemshuka!.
Alama ya kuuliza (?)
Alama hii hutumika kama ifuatavyo:-
(a) Hutumika kuuliza maswali.
Mfano: Mwalimu leo tutafanya mtihani?
Alama ya mabano [ ( ) ]
Alama hii hutumika kama:-
(a) Hutumika kuonesha maana ya ziada katika sentensi.
Mfano: Wale watoto wangu (Robson, Karen, na Maurene) nawapenda sana.
Alama ya kistari ( - )
(a) Alama hii hutumika kuonesha kuwa neno linaendelea katika mstari unao fuata-------
Mfano: wafanya ka-
zi wa shu-
le wote.
(b) Hutumiwa kuzungumza maneno au kujenga neno moja na mtindo huu hutumika zaidi katika maneno yenye asili ya kigeni.
Mfano: Idd - Al- Haji
Dar – Es – Salaam
(c) Hutumika kuunganisha sentensi mbili, sentensi ya pili ikiwa ni ufafanuzi wa sentensi ya kwanza.
Mfano: Tulipofika hifadhi ya manyara, tuliwakuta simba wamelala – simba dume, jike na watoto wanne.
(d) Hutumika badala ya nukta mbili.
Mfano: Nenda kanunue –dagaa, muhogo, maharage, kuni .
Alama ya mtaja ( “ ” )
(a) Hutumika katika kukazia maneno aliyosema au aliyoandika mtu mwingine.
Mfano: “Mwalimu Nyerere alisema, “Enzi za utawala wangu nilifanya mambo mengi mazuri na mengine ya kujenga kwa kuwa nchi yetu ilikuwa bado changa. Lakini cha kushangaza ninyi mmechukua mambo ya kijinga niliyofanya na mnaacha mazuri niliyofanya. Serikali imeshindwa hata kukusanya kodi!
(b) Hutumika kubainisha maneno ya kigeni yanayotumika katika lugha fulani.
Mfano: Ilituwia vigumu “kujiexpress” mbele za watu.
Tumefikishana mahakamani tatizo ni ugomvi wa “kiamba”
(c) Hutumika kubainisha maneno ya msimu katika lugha fulani.
Mfano: “Alipomcheki” aligundua kuwa ni “changudoa”
Ritifaa / kibainishi (‘ )
(a) Kutofautisha “ng” na “ng” katika baadhi ya maneno .
Mfano: ngambo - n’gombe ng’ambo
Ngangania - ng’ang’ania
Ngarisha - ng’arisha
(b) Kuonesha kuwa herufi fulani imeachwa katika neno.
Mfano: Vuta N’kuvute - vuta n’kuvute
Watoto wa mama N’tilie -
Nukta katishi / nukta dukuduku ( ………..)
(a) Hutumika kubainisha mdokezo.
Mfano: Nakupenda sana lakini…………………
(b) Hutumika kuonesha kuwa kuna maneno yaliyotangulia katika tungo.
Mfano:………………fika ofisini mara moja.
Matumizi ya herufi kubwa
(a) Hutumika kila mwanzo wa sentensi
Mfano:- Mama njoo
(b) Hutumika baada ya alama ya nukta, kuuliza, kushangaa.
Mfano: “Nani huyo?” Aliuliza mama.
Wewe ndiyo! Mwanga sana wewe.
(c) Hutumika kutaja majina ya kipekee
Mfano: Winnie, Abel, Ade, Marco, Concepta, Manoza.
(d) Majina ya dira
Mfano: Mashariki, Kaskazini
(e) Majina ya vyeo
Mfano: Sheikh, Rais, Mwenyekiti
(f) Ufupisho wa vyama, mashirika, jumuiya
Mfano: UN, CHADEMA, HKL, ECOWAS
(g) Majina ya vitabu na mada …..
Mfano: “JE, TUTAFIKA?” “USHUHUDA WA MIFUPA”, Mfadhili.
(h) Majina ya sikukuu
Mfano: Krismass, siku ya wapendanao
(i) Majina ya nafsi yanapotumika kuleta maana maalum.
Aya
Ni jumla ya sentensi zinazoelezea wazo moja na hufanya kazi zifuatayo:-
(a) Hueleza au kufafanua wazo maalum
(b) Kuwa na mawazo yaliyo katika mantiki
(c) Kuwa na mifano ya kutolea ufafanuzi.
Mkwaju ( / )
Kutenga maneno mawili yenye maana sawa yanapotumika kwa pamoja.
Mfano: mofimu ya njeo / wakati
Hutumika kutenga namba za kumbukumbu na tarehe.
Mfano: Kumb. 03/DA/20078
11/08/2014
INSHA
Insha ni maandishi au masimulizi juu ya jambo au kitu fulani. Uandishi wa insha huwa katika aya.
MADHUMUNI YA UANDISHI WA INSHA
Kujua ni jinsi gani mwandishi anaweza kujitegemea katika kuwaza na kujenga mawazo yake kwa makini.
Kujua ni jinsi gani mwandishi anaweza kuandika mawazo yake kwa ufupi au kwa urefu kwa watu wengine.
MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA UANDISHI WA INSHA
Kuweka vidokezo vya msingi vinavyohusiana na habari uliyopewa.
Kugawanya insha katika aya mbalimbali.
Kuwa na mpangilio mzuri wa matumizi ya maneno.
Kutumia lugha inayoeleweka.
Mpangilio mzuri wa mawazo wenye kuzingatia mantiki.
Kutokutumia lugha ya mkato
Kutumia msamiati wa kutosha.
Kuzingatia sarufi ya lugha
Kuzingatia matumizi ya alama mbalimbali za uandishi.
kuhakikisha insha inafuata na kujali matumizi ya nyakati mbalimbali.
Insha lazima iwe na sehemu kuu tatu:- Mwanzo
- Kiini
- Mwisho
12. Lazima kuwa na utangulizi mzuri unaovuta umakini.
13. Kuandika kiini cha insha kwa mpangilio unaofaa na kila wazo lipewe aya yake.
AINA ZA INSHA
Kuna aina nyingi za insha lakini zinaweza zikawekwa katika makundi makuu mawili,
(i) Insha za wasifu / kitawasifu
(ii) Insha za hoja
NB: Baadhi ya wataalam huzigawa insha katika makundi makuu matatu.
(i) Insha za wasifu
(ii) Insha za kisanaa
(iii) Insha za hoja.
Nini maana ya insha za wasifu:-
Insha za wasifu ni insha ambazo huelezea sifa za kitu, hali au mtu fulani. Sifa zinaweza zikawa nzuri au Mbaya
Insha za Hoja:-
Hizi ni insha ambazo hutetea mawazo ya aina fulani na kupinga mengine kwa uthibitisho dhahiri.
Insha za kisanaa;-
Hizi ni insha ambazo hutumia vipengele mbalimbali vya kifasihi katika kuwasilisha ujumbe. Mbinu hizo ni kama vile nahau, methali, misemo, tamadhali za semi na mbinu nyingine za kisanaa.
NB: Insha zisizo za kisanaa ni insha ambazo hazitumii lugha ya kifasihi katika kufikisha ujumbe wake.
MUUNDO WA INSHA
Insha kwa kawaida hugawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni:
Utangulizi / Mwanzo wa insha
Kiini cha insha / kati
Mwisho wa insha / hitimisho
MWANZO WA INSHA
Katika sehemu hii inapasa kuwa na maelezo mafupi yanayozingatia fasihi ya jambo linalozungumzwa, uhusiano wake na vitu vingine na muhtasari wa insha inayotungwa.
NB: Kwa kawaida utangulizi huwa na aya moja
2. KIINI CHA INSHA
Hii ndiyo sehemu muhimu zaidi katika insha ambayo huzingatia mawazo makuu na kupangwa katika aya zenye mtiririko wa mantiki wa mawazo. Ufafanuzi wa mawazo makuu kuzingatia kichwa cha habari cha insha, mifano dhahiri kutumia kuonesha uhalisi wa jambo linalofafanuliwa.
3. HITIMISHO
Katika sehemu hii kunakuwa kuna msisitizo wa yale yaliyojadiliwa, msimamo, maoni au mapendekezo kuhusu jambo linalozungumzwa.
NB: Mara nyingi hitimisho huwa ni muhtasari wa yaliyozungumzwa katika insha. Insha ni lazima ianze na kichwa cha habari na kuandikwa kwa herufi kubwa, juu katikati ya insha. Kichwa cha habari kiwe kifupi na kijitosheleze. Mara nyingi maneno yasizidi matano (5), ni vizuri kichwa cha habari kipigiwe mstari.
NB: Ni vizuri insha ikazingatia idadi ya mawazo.
UTUNGAJI WA BARUA
(i)kipengele cha uandishi wa Barua, mambo yafuatayo yazingatiwe
. Afuate ufafanuzi wa kila aina ya Barua kwa kufuata mpanglio sahihi yani
(i) Barua za kirafiki
(ii)Barua za kiofisi / kikazi
(iii) Barua za simu
(iv) Barua za mialiko.
(v) Barua za magazeti
(vi) Barua za kutoa taarifa.
* Mifano iongezwe katika ya kikazi na magazeti.
*katika Barua za mwalik0 mfano utolewe uonyeshwe.
*utungaji wa matangzo mfanoitolewe / uonyeshwe.
1. Barua za Kiofisi:-
Hizi ni barua rasmi ambazo huandikwa kwa madhumuni mbalimbali kama vile kuomba kazi, kutuma na kupokea taarifa rasmi, kuomba nafasi ya kusoma, kuomba likizo, kuomba uhamisho.
MAMBO YA KUZINGATIA
(i) Anuani ya mwandishi ambayo hukaa juu upande wa kulia.
(ii) Tarehe inayokaa chini ya anuani ya mwandishi
(iii) Anuani moja au zaidi ya mwandishi inayokaa upande wa kushoto baada ya kumbukumbu namba
(iv) Salamu “Ndimi”
(v) Barua yenyewe ufafanuzi wa kusudio la barua
(vi) Mwisho wa barua
(vii) Sahihi ya mwandishi
(viii) Jina la mwandishi (kamili)
(ix) Cheo cha mwandishi.
Mfano:
MTAA WA MTAKUJA,
S.L.P 14631,
MAJENGO – MOSHI.
13/11/2012.
MENEJA MKUU,
KIWANDA CHA MATOFALI,
S.L.P 87,
MOSHI.
Ndugu,
YAH: OMBI LA KUJA KUJIFUNZA KUFYATUA MATOFALI
Kichwa cha habari hapo juu chahusika . Sisi ni kikundi cha vijana kumi na tano (15) ambao tumeamua kujiarijiri wenyewe kwa kufanya kazi ya kufyatua matofali.
Tunaomba kutembelea kiwanda chako kwa lengo la kujifunza zaidi.
Ni matumaini yetu kwamba ombi letu litakubaliwa.
Wako mtiifu,
………………….
Vai Selis Chalamila
(Katibu wa kikundi)
2. Barua za magazetini
Hizi ni barua ambazo huandikwa na wasomaji mbalimbali wa magazeti na kupelekwa au kutumwa kwa mhariri wa gazeti husika.
MADHUMUNI:-
- Kupongeza kuhusu jambo fulani
- Kufichua maovu fulani
- Kutoa maoni / mapendekezo kuhusu jambo fulani
MAMBO YA KUZINGATIA / MUUNDO
Kuwa na kichwa cha barua ambacho huandikwa mwanzoni kwa herufi kubwa au kwa wino mzito.
Mwanzo wa barua ambao huanza na “Ndugu Mhariri,” Lazima kuwe na salamu.
Barua yenyewe na huwa na ufafanuzi wa hoja kwa kutolewa katika sehemu hii.
Mwisho wa barua mara nyingi huwa na maoni, maombi au mapendekezo.
Jambo la mwisho ni jina la mwandishi, anwani, na tarehe. Hivi huandikwa chini ya barua upande wa kushoto.
Mfano:
SHULE ZITUMIKE KUKUZA VIPAJI
Ndugu Mhariri,
Miaka ya nyuma swala la kukuza michezo shuleni lilikuwa linapatiwa kipaumbele. Hii ilidhihirishwa na kila shule kuwa na viwanja kwa ajili ya michezo mbalimbali.
Kwa miaka ya karibuni mambo siyo hivyo tena kwenye baadhi ya shule, viwanja hivyo vimeongezwa majengo kiasi kwamba sasa kunabakia sehemu finyu kwa ajili ya kufanya michezo hiyo. Wanapolazimika kufanya hivyo hutakiwa kwenda eneo la mbali, jambo ambalo linakuwa sio rahisi kulitekeleza mara nyingi.
Hata hivyo, kwa ushauri wangu naona kuwa shuleni ambapo wanafunzi bado ni wadogo wana nafasi nzuri ya kuendeleza vipaji vyao vya michezo.
Hii inawezekana sio kwa kusoma darasani bali kwa kufanya mazoezi ya michezo husika.
Tunaomba waalimu na mamlaka husika waliweke hilo maanani ili vijana waweze kweli kukuza vipaji vyao vya michezo. Ni kwa njia hiyo pekee ndiyo tutaweza kupata wanamuziki bora, wanariadha makini, waigizaji hodari wacheza mpira wa kiwango kinachoastahili na mabondia wa kiwango cha kimataifa. Hapo tunaweza tukawapata wakina Filbert Bayi wapya, wakina Abdallah Kibasen wapya, akina Mbaraka Mwishekhe wapya nk.
Fausta John,
S.L.P 514,
3. Barua za Mialiko
Ni barua ambayo aghalabu huandikwa kumualika mtu katika jambo fulani mfano harambee, sherehe, mkutano, semina, dhifa, warsha, kongamano.
MAMBO YA KUZINGATIA:-
(i) Jina la mwandishi na anuani yake
(ii) Jina la mwandikiwa / mwalikwa
(iii) Lengo la mwalikaji kwa ufupi
(iv) Tarehe ya mwaliko
(v) Mahali pa mwaliko
(vi) Siku na wakati wa kukutana
(vii) Mahali pa kupeleka jibu
MFANO:-
Bwana na bibi John wanayofuraha kukualika bibi Vai kwenye shehere ya kumpongeza mtoto wao mpendwa Samweli kwa kumaliza darasa la saba, siku ya Jumapili tarehe 28/07/2013 kwenye ukumbi wa Uhuru Park Majengo saa kumi jioni.
Jibu kwa:
Emerco Mashelle
0713 – 208123
NB: Wakati mwingine barua za mialiko huandikwa kama barua za kindugu ila huwa na maneno machache ili zisipoteze lengo maalumu.
MFANO:
Kijiji cha Kafule,
S.L.P 15,
Itumba – Mbeya
18/07/2013
Kwako mpendwa Vai,
Salam, Tarehe 11/08/2013 ninaadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwangu, nakualika ufike tufurahi pamoja kwenye chakula kuanzia saa tano usiku nyumbani kwangu, Tafadhali naomba unijibu. Kufika kwako ndiyo furaha yangu
Rafiki yako,
Halima
NB: Kama barua ya mwaliko ni rasmi, yaani ya kiofisi, majina ya mwandikiwa huambatana na cheo chake. Mfano Profesa, Sheik, Mchungaji, Dakrati n.k ambayo hutumika sambamba na maneno ndugu, bwana, na bibi. Wakati mwingine barua za mwaliko huandikwa katika karatasi maalum na kuitwa kadi za mwaliko.
4. Barua za simu
Simu za maandishi ni njia mojawapo ya mawasiliano ya haraka miongoni mwa watu. Mtu anayeandika huipata haraka iwezekanayo kulingana na barua za kawaida. Barua za simu huwa ni fupi, lakini zenye ujumbe uliowazi na unaoeleweka. Ufupi wa barua za simu hutokana na gharama za malipo kwa sababu gharama za simu hulipiwa kulingana na idadi ya maneno yanayoandikwa.
MAMBO YA KUZINGATIA
Anuani ya anayepelekwa taarifa. Hii ni kazima iwe kamili na wazi ili kuziwezesha barua hiyo imfikie mlengwa bila ya matatizo yoyote.
Taarifa au ujumbe. Hiki ndio kiini cha simu, ni vizuri kikaandikwa kwa ufupi na kueleweka, epuka kuandika mambo yasiyokuwa ya lazima.
Jina la mwandishi
NB: (i) Ni vizuri kuandika kwa herufi kubwa kurahisisha usomaji.
(ii) Barua ya simu huandikwa katika karatasi maalumu
(iii) Hakuna barua ya simu ambayo husafirishwa bila kulipiwa.
Mfano: ASHA MWANASEFU SLB 404060 MOSHI
FIKA HARAKA BABA ANAUMWA HAMISI
5. Hotuba
Hotuba ni maelezo ambayo hutolewa na mtu mbele ya halaiki ya watu (watu wengine) kwa madhumuni mbalimbali kama vile kubainisha watu kufanya kazi , kutoa taarifa fulani, kufanya kampeni fulani n.k
SIFA ZA HOTUBA
Hotuba yoyote nzuri ni lazima izingatie mambo yafuatayo:-
(i) Ukweli wa habari na taarifa inayotolewa.
(ii) Ufasaha wa lugha ili kuifanya hotuba iweze kupendeza na kueleweka vizuri.
(iii) Nidhamu yaani kuwa na adabu njema unapohutubia na unapokuwa
umesimama mbele ya watu.
(iv) Mantiki nzuri yaani mfuatano mzuri wa mawazo na fikra.
(v) Sauti ya kusikika wazi pamoja na ishara zinazoeleweka iwapo hotuba inatolewa mbele ya watu.
AINA ZA HOTUBA
(i) Mahubiri
Hizi ni hotuba zinazohusu mafundisho ya dini na hutolewa makanisani, misikitini, mbele ya waumini na pia kwa njia ya redio au televisheni.
(ii) Hotuba za kisiasa na za kiserikali
Hizi ni hotuba zinazohusu mambo ya kiserikali na vyama vya siasa kwa lengo la kufafanua maazio au sheria, kampeni za kisiasa, kuhimiza watu kutenda jambo fulani n.k.
(iii) Mihadhara au masomo ya darasani:-
Hizi ni hotuba au mafundisho yanayotolewa na waalimu shuleni hasa wanapokuwa wanafundisha kundi kubwa la wanafunzi hasa vyuo vikuu.
(iv) Risala
Hii ni hotuba au taarifa fupi ambayo husomwa mbele ya kiongozi kwa niaba ya kundi fulani la watu ili kutoa maelezo au kuonesha msimamo wa kundi hilo kwa kiongozi husika.
NB: Baada ya kusomwa , kwa kawaida risala hiyo hukabidhiwa kwa mhusika katika maandishi kama kumbukumbu ya kudumu.
MUUNDO WA HOTUBA
Kwa kawaida hotuba huwa na muundo ufuatao:-
(i) Mwanzo
- Huwa na salamu ambazo hutegemea hadhara iliyopo na lengo la hotuba.
(ii) Utangulizi:-
- Huwa na utambulisho kulingana na vyeo vya hadhara iliyopo.
Mfano; Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waheshimiwa wabunge, Waheshimiwa madiwani, Waheshimiwa wakuu wa shule, Waheshimiwa Waalimu, mabibi na mabwana
NB: Katika utambulisho kunaweza kuwa na shukrani pamoja na muhtasari wa hotuba itakayotolewa.
(iii) Kiini cha hotuba / kati
- Sehemu hii ndiyo hutoa ujumbe kwa wasikilizaji na ndiyo sehemu muhimu zaidi katika hotuba. Kutoka sehemu hii mhutubiaji hueleza na kutoa ufafanuzi wa yale yote yaliyomsukuma kutoa hotuba kwa hadhira husika.
(iv) Mwisho
- Huwa ni muhtasari wa yale yaliyoelezwa kwa lengo la ….
6. Risala
Kamusi ya Kiswahili sanifu (TUK: 1981) Inafafanua risala kuwa:-
(i) Taarifa inayopelekwa kwa mtu au watu fulani, aghalabu inayoeleza hoja inayotakiwa.
(ii) Hotuba fupi inayosomwa mbele ya kingozi kwa niaba ya kundi fulani la watu ili kutoa maelezo au kuonesha msimamo wa kundi hilo kwa kiongozi.
MUUNDO WA RISALA
Risala huwa na sehemu kuu tatu:-
(i) Mwanzo wa risala
(ii) Kati au kiini cha risala
(iii) Mwisho / hitimisho la risala
MWANZO
Huwa unahusisha utangulizi, salamu, ukaribisho na lengo risala.
KATI / KIINI
Hii ndiyo sehemu muhimu zaidi katika risala , ambapo masuala mbalimbali hufafanuliwa. Mfano: mafanikio, matatizo, changamoto mbalimbali, mapendekezo, maombi n.k
MWISHO
Huwa ni msisitizo wa yale yaliyofafanuliwa kwenye kiini cha risala, shukrani , pamoja na hitimisho.
NB: Kwa kuwa risala huandikwa basi sharti ianze na kichwa cha habari. Tena kiandikwe kwa herufi kubwa na kipigiwe mstari.
7. Matangazo
MAMBO YA KUZINGATIA
(i) Kichwa cha habari (huandikwa kwa herufi kubwa)
(ii) Kutaja aina ya biashara au huduma zinazotakiwa na bei zake.
(iii) Kutaja aina za bidhaa au huduma zinazotolewa na bei zake.
(iv) Kutaja mahali inapotolewa huduma / bidhaa hizo yaani mji, mtaa, kijiji n.k
(v) Kutaja namna ya kuwasiliana
Mfano wa tangazo:-
TANGAZO
Vitabu, Vitabu, Vitabu.
Wale wauzaji maarufu wa vitabu vya Injili/Dini wameleta
Ingizo jipya. Fika dukani kwao Mtaa wa Malapa, Buguruni, Dsm.
Kwa mawasiliano zaidi;
Piga simu zifuatazo;
0765000724
0713000725
UANDISHI WA KAZI ZA FASIHI.
Dhana ya utungaji:
Kutunga ni kitendo cha kutoa mawazo ubongoni kisha kuyadhihirisha kwa kuyaandika au kuyasimulia.
Hatua za Mwanzo za kuzingatia katika kutunga kazi za kifasihi.
i). Kuwa na jambo ambalo unaona linasababisha au lina mvuto kwa jamii.Kisha unafanyia utafiti kujua chanzo chake na kwa nini linaendelea kuwepo.
ii).Baada ya utafiti ni kufanya maamuzi ya njia gani au tanzu gani aitumie kufikisha ujumbe kati ya ushairi , hadithi, semi na maigizo.
iii).Atumie kipera gani kutoa kutoka katika tanzu aliyochagua .Mfano kama ni ushairi atumie nyimbo au ngonjera.
iv).Kulijenga jambo jambo katika fani na maudhui ili kupata mbinu sahihi ya uwasilishaji wa kazi yako kwa hadhira.
v). Mtunzi kujikita hasa katika maudhui ya jambo lako unalotaka kuliwasilisha .Mfano nini dhamira yako.
vi).Mtunzi unaangalia namna ya kuwasilisha maudhui yako, hapa unashughulikia vipengele vya fani yaani muundo , mtindo ,mandhari ,wahusika na matumizi ya lugha.
Hapa mtunzi anatakiwa atumie ufundi na ubunifu wa hali ya juu ili kazi yake ielimishe na kusisimua.
vii).Baada ya fani na maudhui kushughulilkiwa mtunzi aangalie namna ya uwasilishaji wake.Kuangalia kanuni na taratibu za kipera ulichotumia.
viii).Mtunzi unaanza kuandika yale unayotaka kuelimisha jamii kwa kufuata taratibu za uandishi.
ix). Mtunzi unasoma kuangalia kama kile ulichokidhamiria ndicho ulichikitunga.
x).Fanya mazoezi namna ya kuwaslisha hiyo kazi.
Mfano:-
Namna ya kutunga igizo la kifasihi simulizi
i.Kwanza kuteua wahusika watakao sawiri matendo ya tabia zao:-
-Mhusika mkuu hujitokeza mara kwa mara na matendo mengi yanamuhusu yeye.
-Wahusika wadogo huwa wengi.
-Kuteua waigizaji wazuri watakaofanya vizuri katika kuiwasilisha.
-Wahusika wajengwe kwa kuzingatia utendaji wao.
ii.Kuteua lugha itakayotumika.
iii.Kuteua mandhari nzuri katika uwasilishaji wake.
iv.Kuangalia muundo na mtindo wa igizo lake.