Skip to main content




MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI
UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI

FASIHI SIMULIZI:

Fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutumia mazungumzo na matendo katika kuwasilisha ujumbe Fulani kwa watazamaji au wasikilizaji. Mazungumzo hayo huweza kuwa ya kuimbwa
kutendwa au kuzungumzwa, Aina hii ya fasihi imepokelewa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo.

Msimulizi katika fasihi simulizi mbali na kutumia mdomo wake hutumia viungo vyake vya mwili kama mikono, miguu, ishara mbalimbali katika uso wake na hata kupandisha na kushusha sauti yake. Kwa ujumla anaweza kutumia mwili wake mzima katika kuwasilisha na kufanikisha ujumbe wake kwa hadhira yake ambayo huwa ana kwa ana. Isotoshe anafaulu katika kutoa picha halisi ya dhana anayotaka kuiwasilisha kama ni ya huzuni, furaha, kuchekesha n.k.
Zaidi ya kusimulia, kuimba na kuigiza msanii wa fasihi simulizi huwa na nafasi ya kushirikisha hadhira yake kama wahusika katika sanaa yake. Anaweza kutimiza hayo kwa kumfanya mshiriki mmoja kuigiza jambo fulani au kufanya hadhira yote kuimba au kufanya matendo mbalimbali. Ufundi wa aina hii huhitaji umahiri wa hali ya juu. Hali hii humpa msanii wahakiki wake hapohapo.
Kwa upande mwingine hadhira nayo huwa na nafasi na uhuru wa kushiriki au kuuliza maswali pale ambapo hawakuelewa, Vilevile wanapata fursa ya kuonesha hisia zao. Kuhimiza, kukumbushana na kwa hali hiyo fasihi simulizi huwa na uwezo wa kufundisha zaidi. Kwa kuzingatia maoni ya kirumbi (1976) hivyo kutokana na maelezo yaliyotangulia tunaafikiana nae kwamba fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutumia mazungumzo na matendo katika uwasilishaji wa ujumbe ulikusudiwa kwa hadhira. Mazungumzo hayo huwa katika mfumo wa masimulizi, kwa kuimbwa, kutambwa, kughaniwa na kutongolewa.
Fasihi simulizi hueleza jamii kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa, Fasihi huzungumzia mambo ambayo huzunguka jamii husika. Fasihi simulizi huathiri malezi ya watu kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo na matendo.
Fasihi simulizi huenda sambamba na mabadiliko ya jamii na kwa hivyo nayo hubadilika kimaudhui na kifani kufuatia mabadiliko ya mifumo ya KISIASA, KIJAMII na KIUCHUMI. Fasihi simulizi ni utanzu wa kisanaa ulio hai na ambao hukua na kubadilika kutokana na mabadiliko ya wakati na ya mifumo ya jamii.
Hivyo fasihi simulizi ni tukio linafungamana na muktadha (mazingira) fulani ya jamii kutawaliwa na mwingiliano wa mambo yafuatayo:-
a) MSIMULIZI (FANANI)
Huyu ni mtu ambaye anaitamba hadithi, kuimba wimbo kutoa methali au vitendawili.
b) WASIKILIZAJI AU WATAZAMAJI (HADHIRA)
Hawa huwa ni washiriki katika kutazama au kusikiliza fani za fasihi simulizi na mara nyingine huwa wanatumiwa na fanani kama wahusika wa fani yake.
c) MAHALI (MANDHARI)
Hapa ni jukwaa au mahali ambapo tukio la fasihi simulizi linatendeka mahali hapo panaweza kuwa nyumbani, uwanjani n.k.
d) TUKIO.
Ni shughuli ya kijamii ambayo ndiyo muktadha wa utendaji huo wa sanaa mathalani harusi, kazi Fulani, sherehe, msiba, ibada n.k. utendaji huo waweza kuwa katika usimulizi wa hadithi, kutega vitendawili kuimba wimbo/nyimbo au kutoa methali.
e) WAKATI
Ni muda maalumu wa kihistoria au majira maalum ya utendaji huo.

UHIFADHI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Fasihi simulizi inaweza kuhifadhiwa kwenye maandishi na kanda za sauti kwa madhumuni ya kumbukumbu. Tunaweza kutambua fasihi simulizi kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo:-
Kama ilivyoelezwa hapo awali inategemea mdomo wa msimulizi (mtendaji) na masikio ya hadhira.
Fasihi simulizi ni hai kwa sababu inategemea uhusiano wa ana kwa ana wa msimulizi(mtendaji) na hadhira yake kwa hiyo lazima uwepo utendaji wa maneno au wa muziki au wa matendo utakaowasilisha tungo za mtendaji kwa hadhira yake. Utendaji huu hutegemea sana kiimbo shadda milio na vihisishi.
Fasihi simulizi inatendwa hivyo lazima iwe na mtendaji. Huyu anaweza kuwa mwimbaji, msemaji au mtendaji. Kazi yake ni kuanzisha au kueneza tungo au kazi zote mbili. Mtendaji huyu hutumia vifaa vya kusikika au kuonekana katika kujieleza, kwa mfano wimbo toni za miondoko kwa njia hii anakuwa karibu sana na hadhira yake.
Kwa kuwa kila mtu anaweza fuatilia kwa kiasi na kwa kuwa fasihi simulizi inategemea kumbukumbu za mtu binafsi hadhira inapotumia na kueneza tungo za fanani pia huimbwa usanii na kuzijenga tungo hizo kwa namna zao. Jambo hili hufanya kazi ya fasihi ielezwe kwa namna kadha kutegemea mazingira na masimulizi.
Kukabiliana na hadhira moja kwa moja kuna athari katika tungo za fasihi simulizi, fanani huweza kubadilisha tungo katika utendaji wake kadri apendavyo ili mradi akuze uzuri wa kazi yake au alete athari Fulani inayokidhi haja ya wakati ule.
Mwambatano wa tungo na mazingira maalum ni muhimu mazingira huathiri sana usanii wa tunngo na maudhui yake. Zipo tungo ambazo huambatana na matukio maalumu na hata kama zimepitwa na wakati huweza kugeuzwa zikasadifu kipindi mahususi.
Fasihi simulizi ina tabia ya uhai na hutegemeana na sanaa za maonyesho na ghibu yaani sanaa ya muziki, Tabia hii inaitwa hali ya utegemezi. Hii ni kwa sababu huchota uhai wake kutokana na vitendo na vitabia vya fanani, mahadhi, toni za muziki na vipengele vingine vya sanaa za maonyesho.
Bila kuzingatia vipengele hivi vya utendaji kazi ya fasihi simulizi inaweza kuchapwa kwa mfano bila mahadhi, madoido, upigaji ngoma, miondoko ya uchezaji na mazingira ya tukio unamotumiwa wimbo unaweza kukosa uhai wake.
TANZU ZA FASIHI SIMULIZI
Kuna makundi mawili muhimu ya tanzu ya fasihi simulizi, kundi moja linahusu tanzu zenye mwelekeo wa kishairi na kundi jingine linashughulikia tanzu za kinathari au zenye sifa za kihadithi.
Tanzu za kishairi zina sifa nyingi za ushairi kuliko tanzu zenye lugha ya kinathari, Ushairi aghalabu hutumia lugha ya kitamathali na mkato. Pia ushairi una mizani ulinganifu wa sauti na mapigo.
Matteru (1987) amesema kwamba katika muktadha wa fasihi simulizi zenye kutumia mapigo kwa utaratibu maalumu. Mapigo haya yanaweza kuwa ya muziki au yoyote yale yaliyopangwa kwa muwala wa uwazi.
Tanzu kama nyimbo, maghani, methali, vitendawili, misimu hupatikana katika kundi hili la ushairi, Kwa upande mwingine matteru (1987), anasema kwamba tunzu za kinathari zinajumlisha tungo zote za fasihi simulizi zenye kutumia lugha ya kawaida. Matteru anamlizia kwa kusema kuwa “nathari” hujumlisha tanzu na fani kama hadithi, ngano, tarihi, visasili, vigano, masimulizi.
MASIMULIZI / HADITHI
Tanzu mbalimbali za hadithi zinaingia hapa, mfano ngano, hekaya n.k. simulio la kihistoria na la kiasili kama vile VISAKALE (Masimulizi ya kimapokeo/wahenga/ mashujaa), kumbukumbu, VISASILI (hadithi za zamani zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii).
Hadithi au masimulizi ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari pia mtiririko wake huwa mwepesi na sahihi. Zipo hadithi za kubuni na za kihistoria.
UMUHIMU WA HADITHI KATIKA FASIHI SIMULIZI
i. Hutumiwa kuipa jamii mwelekeo. Simulizi au hadithi hufumbata mtazamo wa jamii pamoja na falsafa yake nzima na ndiyo kielezi cha jamii husika.
ii. Hutumiwa kuyaendeleza maadili ambayo huwa kama nguzo kuu ya wanajamii. Kila hadithi huwa na funzo maalum.
iii. Huonya, huadhibu, huelimisha, huishauri na kuinasihi jamii kupitia wasifu wa wahusika.
iv. Simulizi au hadithi hutumika kuirithisha jamii elimu thamani na amali muhimu kutoka kizazi hadi kizazi. Tanzu za fasihi simulizi huwa nyezo kuu ya kurithisha elimu ya jadi katika jamii husika.
v. Hutumiwa kama burudani
vi. Hutumiwa kuendeleza uhusiano uliopo kati ya wanajamii na hasa uhusiano wa kushirikiana tofauti na usomaji wa vitabu.
vii. Hukuza uwezo wa watoto kuyakumbuka mambo. Huboresha uwezo wao wa kumbukumbu n.k.
KUHAKIKI KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Sifa kuu za kimtindo zinazotumika katika uhakiki wa hadithi / simulizi ni:-
i. DHAMIRA NA MAUDHUI
Ndani ya dhamira tunapaswa kulitambua wazo kuu au lengo kuu la hadithi ni jumla ya mambo yaliyomo ndani ya hadithi hiyo, yanayoibuka katika kuuendeleza wazo hilo kuu.
ii. MSUKO
Huu ni muundo wa hadithi yenyewe, Hapa tunaangalia jinsi matukio ya hadithi yalivyopangwa kuanzia mwanzo kwenye kitangulizi. Mvuto wa hadithi ambao mgogoro kati ya wahusika waliopo. Kuwepo kwa taharuki, harakati zao hadi kwenye kilele cha hadithi au upeo na hatimaye mwisho wake.
iii. USISIMUZI
Hapa tunachunguza uwezo wa hadithi wa kuweza kuiteka hadhira yake.
iv. URUDIAJI
Kwa kawaida urudiaji unaweza kuwa wa vipengele vya muundo, mfano: virai, maneno, sentensi, vifungu fulani, nyimbo n.k. pia huwepo urudiaji wa mawazo, fikra, maoni n.k . Sababu za urudiaji huwa ni kufanya mambo yaliyozungumzwa kukumbukia au kusisitiza jambo fulani.
v. MATUMIZI YA NYIMBO
Nyimbo hutumika kwa kiasi kikubwa katika hadithi na kufanya kazi zifuatazo:-
Kuonyesha au kusisitiza kiini au wazo kuu katika hadithi au simulizi inayohusika.
Hushirikisha hadhira katika hadithi inayotambwa.
Huongeza uhai wa usimulizi kwa kushirikisha hadhira.
Huwapambanua wahusika mbalimbali wanaopatikana katika hadithi hiyo.
Kuondoa ukinaifu unaotokana na kuutumia mtindo wa aina moja kwa kipindi kirefu.
Kuwazindua wasikilizaji ambao huenda wakawa wamelala au kusinzia wakati hadithi inatambwa.
Hutumika kama kiliwazo katika hadithi za kitanzi
vi. VILIWAZO / UCHESHI
Ni sehemu ya hadithi ambayo huwa imekusudiwa kuituliza hadhira kidogo hasa kwenye hadithi zinazozungumzia masuala ya kusikitisha au ya kitanzia, Kiliwazo kinaweza kuwa kifungu kilichojaa ucheshi kilichokusudiwa kuondoa kwa muda ile hali ya kusikitisha. Nyimbo hutumiwa pia kama kiliwazo.
vii. TAMATHALI ZA SEMI
Hadithi huwa na ufundi wa kisanaa ambao hujitokeza kwa matumizi ya lugha yenye mvuto na iliyochanganya matumizi ya tamathali mbalimbali za semi. Mfano sitiari, tashibiha, tashititi, tashihisi, tafsida n.k
USIMULIZI – HAKIKI / TUNDUIZI
Mtambaji wa hadithi hutoa maoni kuhusu hadithi anayoisimulia. Msimulizi anaweza kutoa maoni yake kuwahusu wahusika wanopatikana hadithini au kuyahusu matukio fulani yaliyoko hadithini, kwa kiasi fulani huweza kuathiri usimulizi huu.
ix. WAHUSIKA
Kuna wahusika wa aina mbili katika hadithi. Wahusika binadamu na wahusika wanyama ambao wanapewa sifa za binadamu (mazimwi, majitu n.k.)
Katika usimulizi wa hadithi, mpaka ulipo kati ya ulimwengu wa kawaida wa binadamu na wanyama hufutwa.
Binadamu wanoweza kulingana, kujadiliana, kuzungumza na kuhusiana kwa jumla na wanyama. Katika hadithi simulizi wanyama wakubwa huweza kushindwa na wanyama wadogo. Hii ni namna ya kuwakejeli wasiotumia akili zao. Viumbe wakubwa wa kudhaniwa kama mazimwi majitu husawiri kama viumbe wanaoongozwa na tamaa kubwa, ulafi na uovu ulikithiri. Hii ni njia mojawapo ya kuziakisi sifa ambazo zinaonekana mbaya katika jamii.
Aidha kuna hadhira za aina mbili hadhira tendi na hadhira tuli. Hadhira tendi hushiriki katika usimulizi wa hadithi mfano katika nyimbo kupiga makofi, kucheza, kuitikia, kubadilisha wasimuliaji, kuuliza, kujibu maswali na kucheza. Hadhira tuli yenyewe huwa haishiriki kwa namna yoyote ile inasikiliza tu.
x. TANAKALI SAUTI
Mtambaji katika utambaji wake huweza kutumia sauti ambazo zinaeleza hisia au kuchora picha ya kutokea kwa jambo fulani.
Pia hutumiwa kutia utamu, mvuto na msisimko wa lugha ya mtambaji, mfano mara cheche akatwaa zumavi akapiga, kanga pia singizia moto ,ti,ti,ti......., nikamtwaa nikamfungafunga na majani ya mgomba nikampiga pu, pu, pu,...
xi. ISHARA NA TASWIRA
Ishara ni matumizi ya vitu Fulani kuvisimamia vingine yaani huashiria vitu vingine tofauti.
Mfano:- mti mkubwa kuashiria uhusiano uliopo kati ya watu na miungu katika jamii kadhaa.
Taswira ni matumizi ya lugha ambayo inamfanya msikilizaji au hadhira iweze kuunda picha akilini. Mtumiaji anaweza kutumia picha au tamathali za semi. Mfano sitiari kuunda picha hizi.


xii. UTOKAJI KANDO
Ni mbinu ambayo mtambaji au msimulizi anatoka kando ya utambaji wake na kutoa maoni kuhusiana na kitu kisichohusiana na hadithi moja kwa moja.
Kuna utokaji kando wa nje ambao unatokana na sababu zilizo nje ya hadithi yenyewe, mfano kutokana na hadhira
Utokaji kando ambao inasababishwa na nia ya kutoa maoni kuhusu tukio fulani au kitu Fulani katika hadithi yenyewe mfano kutokana na hadhira.
Utokaji kando ambao unasababishwa na nia ya kutoa maoni kuhusu tukio fulani au kitu fulani katika hadithi yenyewe. Huu ni utokaji kando wa ndani. Hii inahusiana na usimulizi tunduzi.
MAIGIZO(DRAMA ) SANAA ZA MAONESHO
Maigizo yanatumia watendaji kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani. Ni sanaa inayopatikana katika makabila.
Drama za kiafrika huambatana na ngoma, utambaji, hadithi, nyimbo na matendo ya kimila (jando na unyago), kuna maigizo yanayofungamana na michezo ya watoto, matanga, uwindaji, kilimo n.k.
MAIGIZO YA WATOTO
Watoto wanapocheza hufanya maigizo ya matendo ya kimaisha wanayoyaona katika jamii zao mfano kulima, kufanya biashara, harusi, matanga n.k. hizi ni sanaa za maonesho zenye kuwaburudisha na kuwaelimisha watoto licha ya kukuza vipaji vyao vya ubunifu.
MAIGIZO YA MSIBANI
Katika baadhi ya makabila, watani au wajukuu wa marehemu hupaswa kufanya maigizo yanayohusiana na maisha, matendo au tabia za marehemu. Hii huwapunguzia wafiwa huzuni yao mbali na kutoa mafunzo fulani kwa watu waliopo msibani, Mfano tabia mbaya, maigizo hayo hupinga tabia mbaya.
MAIGIZO YA SHEREHE
Sherehe kuu za jamii ni kama vile kuzaliwa kwa mtoto, mtoto kupewa jina, jando na unyago, harusi, kubadilisha rika, kuanua matanga, sherehe za kisiasa (mfano kutawazwa kwa mtemi), sherehe za kidini (mfano kuwakaribisha mwezi mwandamo) n.k. kila sherehe huwa na sanaa zake za maonesho ambazo wakati mwingine huambatana na maigizo.
MAIGIZO YA KIDINI
Maigizo hayo hufanywa wakati wa ibada, matambiko na shughuli nyingine za kidini katika maigizo ya aina hiyo mzimu au miungu huwa ndiyo hadhira ya igizo linalofanyika.
Uigizaji ni muhuimu sana katika fasihi simulizi katika uigizaji huu watendaji huiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kutoa ujumbe fulani. Uigizaji huu unaweza kuwa na nia ya kukejeli, kudhihaki, kukosoa au hata kuwaburudisha. Uigizaji hautegemei sauti tu bali pia maliba mahususi kama majusoo au Barakoa (maski) pamoja matendo yasiyoambatana na sauti kama michezo bubu ambayo inatilia mkazo mkubwa kwenye matendo.
Utambwaji wa hadithi unawasilishwa kwa hadhira kwa utendaji wa kisimulizi/ kitambwaji mashairi ni uigizaji au dhana ya aina Fulani.
Mvinga ni sherehe za kiutamaduni na huweza kuhusisha matambiko, miviga hufumbata maigizo ya aina fulani kutegemea sherehe inayohusika.
VITANZU AU VIPERA VYA MAIGIZO AU DRAMA
i. MICHEZO YA JUKWAANI
Hapa pana mpangilio na mazungumzo baina ya watu na matendo yao, mazungumzo hayo hujenga kisa ambacho kinaonesha mgogoro fulani, kuna aina ya michezo inayoambatana na sauti na isiyoambatana na sauti kama vile ucheshi bubu, michezo bubu n.k.
Onyesho bubu, Kimsingi vitanzu hivi huhusisha utendaji ambao unategemea matumizi ya ishara za mikono na sehemu nyingine za mwili pasipokuwa na maneno.
ii. MAJIGAMBO
Haya ni maigizo ambayo yanaonesha kujitapa (yaani kujigamba) kwingi kwa mtu ambaye labda ni shujaa au ambaye ametenda mambo ya kishujaa au yenye uzito fulani. Wahusika wanaopatikana katika majigambo ndiyo watambaji au wasimuliaji wa majigambo yenyewe. Ni kawaida ya majigambo kuwa na lugha nzito iliyojaa tamathali yenye taswira au picha za undani na yenye nia na mawazo mazito.
iii. VICHEKESHO
Ni mpangilio wa maneno ambayo yanawasilisha ujumbe fulani maalum kwa njia ya kuchekesha au kufurahisha. Kimuundo vichekesho huwa vifupi na havihitaji uchambuzi mpevu au wa ndani ili kupata maana nyingine ya ndani. Lugha yake huweza kuwa nyepesi na iliyojaa picha ambazo watazamaji wana uwezo wa kuzitambua.
iv. NGONJERA AU USHAIRI WA KIMASEMEZANO
Ngonjera ni mpangilio wa tungo za kishairi za kujibizana. Ili ushairi huu uwe sehemu ya majibizano lazima uambatane na utendaji yaani wanaohusika wanaotumia ishara za mikono, mwili, ishara za uso na nyingine ili kuwasilisha ujumbe wao. Ikiwa ngonjera haziambatani na matendo au utendaji haziwi tena sehemu ya maigizo bali sehemu ya ushairi. Mshairi mmoja anaweza kutongoa au kutunga ubeti na kutenda matendo yanayoambatana na kiini cha ubeti wako, ngonjera, huweza kutumiwa kuwatia watazamaji au hadhira hamasa ya kutenda jambo au hata kuwasilisha maarifa fulani kwao.....
v. MAZUNGUMZO
Mazungumzo ni maongezi ya kimajibizano yanayotokea baina ya watu wawili au zaidi kigezo kikuu cha kuyafanya yawe ya kifasihi ni kuwapo kwa usanii na ufundi katika muundo wake na jinsi yanavyowasilisha ujumbe wake. Hapo juu tumeona mazungumzo ni sehemu muhimu ya michezo ya jukwaani lakini yanaweza pia kuangaliwa kivyake.
Katika jamii nyingi mazungumzo hupatikana kwa njia mbalimbali. Njia kuu za kimisingi ni kuwako kwa hotuba, malumbano kati ya watani, ulumbi au usemaji wa kiufundi wa wanajamii tofauti na pamoja na mawaidha. Hivi ni vipengele vyepesi kueleweka kwa sababu vimeenea katika jamii nyingi.
VIPERA VYA TANZU YA HADITHI KATIKA FASIHI SIMULIZI
NGANO
Hizi ni hadithi za kimapokeo zinazotumia wahusika kama vile wanyama, majoka, binadamu, mawe, miti n.k.
Fanani wa ngano hutumia maneno ya kuvuta hadhira kwa vile huanza na PAUKWA...... ambapo hadhira hujibu PAKAWA. Fanani huanza kusimulia hadithi yake baada ya utangulizi ambao huwavutia, huwachangamsha na kuwafanya waache kazi nyingine au kusinzia na kusikiliza ngano hiyo.
Mtambaji wa ngano wakati akiendelea kuhadithia anaweza kuuliza hadhira yake kama “niendelee? au nisiendelee? Kauli hiyo huwafanya hadhira wasisimke na kuuitikia kwa sauti” ENDELEA!!!. Ngano hufuata muundo rahisi na wa moja kwa moja. Kwa kawaida lengo kuu la ngano ni hadithi ya kuwaasa watoto ndiyo maana humalizia kwa kuwatia moyo kama vile wakaishi kwa raha mstarehe, wakazaa na kuzaa, maisha yakawa mazuri, amani ikatawale n.k.
ii. TARIHI(VISAKALE)
Hizi ni hadithi ambazo husimuliwa kutokana na matukio ya kihistoria. Matukio hayo yanaundwa kisanaa ili kuvutia watu katika jamii. Tarihi inahusu matukio yanayoweza kuwa ya furaha au huzuni na ni ya kusisimua ili kuwakumbusha watu walikotoka. Fanani wa tarihi mara nyingi pia huanza kusema “paukwa”na hadhira kuitikia “pakawa”. Kuna baadhi ya masimulizi ya tahiri ambayo huanza kwa nyimbo au majigambo ambayo huwafanya wasikilizaji kuwa makini na matukio yanayosimuliwa. Mara nyingi wahusika wa tarihi ni binadamu ambao hupewa uwezo mkubwa au mdogo mno ili kuyakinisha matukio yanayozungumziwa na kuyawekea mantiki. Tahiri anaweza kusimulia kuhusu historia ya mfalme, koo za kitawala, kumbukumbu za kutokea kwa ukoo Fulani, magonjwa, vita, njaa.
VISASILI
Hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusu asili ya ulimwengu na mwenendo wake, kuhusu asili yao wenyewe, maana na shabaha ya maisha yao. Hadithi hizi husimulia mambo yanayohusiana na maumbile ya watu, wanyama, miti na vitu visivyo na uhai.
Wahusika wa visasili ambao si binadamu hupewa hadhi na uwezo wa binadamu. Kwa mfano hadithi inayohadithiwa chanzo cha chura kuwa na mabakamabaka, au jongoo kuwa na mwili ung’aao na mwororo ni kisasili. Visalili husimulia mianzo au asili ya matendo ya kufkirika, imani au mtazamo fulani katika jamii usimulizi wa visasili pia huambatana na nyimbo.
iv. VIGANO
Ni hadithi fupi zinasimuliwa kwa lengo la kuelezea makosa au uovu wa watu fulani na kutoa maadili yanayofaa. Hadithi hizi hutumia sana nahau na methali katika kutoa maadili kwa hadhira iliyokusudiwa. Maadili hayo hutolewa kama kielelezo wakati wa maongezi au kumkanya mtu.
Wahusika katika vigano ni wanadamu hata wanyama, kwa kawaida vigano hujengwa juu ya tukio moja ambalo hutumiwa kuelezea juu ya maisha halisi katika jamii husika. Mara nyingi vigano havienei sana kwa jamii kwa sababu hutumiwa na muktadha wa mazungumzo.


TAMTHILIYA
TAMTHILIYA NI NINI?
Tamthiliya au drama ni fani iliyokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira fulani, hivyo kwa lugha ya kawaida, tamthiliya huitwa mchezo wa kuigiza. Kwa kawaida tamthiliya huwa na masimulizi ambayo huigizwa na wahusika wa pande mbili au zaidi zinazogongana.
Mgongano huo husababisha mgogoro ambapo unaposuluhishwa na kutanzuliwa, mchezo huwa umemalizika. Tamthiliya ni sanaa ya maneno. Hivyo ina sifa za kawaida za sanaa za maonesho ambazo ni:-
Dhana inayotendeka, watendaji, hadhira, kusudio la kisanaa, uwanja/jukwaa, muktadha wa kisanaa, ubunifu/ umathilishaji,
Tofauti kati ya tamthiliya na sanaa nyingine za maonesho inaelezwa na mlama kama ifuatavyo:-
“Tamthiliya ni aina moja wapo ya sanaa za maonyesho ambazo usanii wa utendaji wa utendaji wake hutegemea zaidi, MATENDO na UONGEAJI, tofauti na aina nyingine kama ngoma ambazo hutegemea zaidi uchezaji ngoma na upigaji muziki. Tamthiliya ni ule utungo ambao unaweza kuwa umeandikwa au haukuandikwa ambao unaliweka wazo linalotoka kuwasilishwa katika umbo la tukio la kuliwezesha kutendeka mbele ya hadhira”.
Kwa mujibu wa maelezo hayo kitu kikubwa kinachoipambanua tamthiliya na sanaa nyingine za maonesho kama vile ngoma, ni msisitizo wake kwenye VITENDO na MAZUNGUMZO YA WAHUSIKA islilahi ya tamthiliya inatokana na neno “mithali” ambalo lina maana ya mfano au ishara ya kitu fulani”.
Hivyo kaitika tamthilia ya kitu kimoja humathilishwa au huwasilishwa na kitu kingnine mathalani katika mchezo wa KINJEKITILE, mwigizaji wa sehemu ya KINJEKITILE huwakilisha muhusika aitwae KINJEKITILE katika mchezo na mhusika huyo wa mchezo huwasilishwa kwa kiasi Fulani KINJEKITILE wa historia.
AINA ZA TAMTHILIYA
Zipo aina nyingi za tamthiliya kama ifuatavyo:-
TANZIA
Tamthiliya ya kijadi ya ulaya ilikuwa na Matawi mawili makuu, TANZIA na KOMEDIA. Tanzia ni tamthiliya ya majonzi kuhusu anguko la mhusika mkuu. Anguko au kifo hicho huweza kusababiswa na udhaifu wake binafsi wa kitabia, kosa fulani alilofanya au mazingira fulani yaliyomzidi uwezo au mchanganyiko wa baadhi ya sababu hizo kwa mfano anguko la kinjekitile na matokeo ya kosa lake binafsi (kuwafanya watu kuyaamini zaidi maji) na mazingira ya kihistoria ( kisiasa na kijamii ambayo hana uwezo nayo)
KOMEDI / RAMSA
Komedi au ramsa ni kinyume cha tanzia. Hii ni tamthiliya inayoishia katika furaha. Mhusika mkuu wa tamthiliya hupambana na matatizo ya kila aina kiasi cha kukaribia kushindwa lakini hatimaye hushinda na kufanikiwa katika malengo yake. Tamthiliya Shakespeare, mabepari wa venisi, shida ni ramsa.
Komedi hupendwa sana na vijana hata watu wazima kwani huwa na mvuto na ucheshi na huweza kuelimisha bila kuleta majonzi au kukatisha tamaa zipo pia tamthilia ambazo zinachanganya sifa za tanzia na komedi.
VICHEKESHO
Vichekesho ni aina ya tamthiliya gezwa au faraguzi (zinazotungwa hapo kwa hapo bila kuandikwa), tamthilya hizi ziliaza miaka ya 1920 kwa lengo la kuburudisha wakazi wa mijini, wakati wa mapumziko.Tamthiliya hizo kwa kawaida zilikuwa na vituko vya kuchekesha na viliwasuta watu waliofikiriwa kuwa WASHAMBA, WAJINGA na WASIOSTAARABIKA.
Hivyo mara nyingi tamthiliya hizo zilimuonyesha mhusika anayetoka shamba na kuja kuzuzuka mjini. Vichekesho viliendelea na hata baada ya uhuru bado vipo ila dhamira zake zilibadilika, Baadhi ya vichekesho siku hizi huigizwa radioni, kwenye televisheni kwenye vilabu vya pombe.
MICHEZO BUBU
Hii ni aina ya tamthiliya isiyotumia maneno, waigizaji hutumia ishara na vitendo tu, na hadhira hujua kinachotokea kwa kuzisoma ishara hizo. Tamthiliya hizi hufaa sana katika jamii zenye mchangnyiko wa watu wasiozungumza lugha moja. Zikiandaliwa vizuri na kuchanganywa na sauti za muziki au ngoma huvutia sana.
DRAMA NGANO
Zipo drama ngao za aina mbili, kwanza ni zile tamthiliya gezwa ambazo watoto au watu wazima huzibuni kutokana na ngano zetu za kiafrika. Ngano au hadithi simulizi huigizwa jukwaani kama drama badala ya kutambwa au kusimuliwa tu. Hii ni njia nzuri sana ya kupata michezo ya vijana shuleni. Watoto wenyewe huweza kuitunga na kuiigiza michezo hiyo kwa kuwa ngano nyingi huhusu wanyama (kwa kujipamba maleba, sauti n.k) ili kuwaigiza wahusika wanaowapenda ( kwa mfano sungura) siku hizi televisheni za ulaya zinatumia sana mbinu hii hususani katika filamu za vikatuni na vikaragosi/wanasesere (puppets).
Aina ya pili ya drama – ngano ni tamthiliya ya kimajaribio zinazojaribu kuigiza fani za jadi za kiafrika katika umbo la tamthiliya za kizungu. Katika tamthilia hizo huweza kuwepo mtambaji ambaye huanza kwa kusema PAUKWA na mwitikiaji akajibu PAKAWA kisha mchezo huendelea kwa njia ya masimulizi na maigizo, mifano mizuri ni tamthiliya za E.Hussein za JOGOO KIJIJINI na NGAO ZA JADI” na tamthiliya za Penina Mhando za “LINA UBANI” na “NGUZO MAMA”.
DRAMA – NGOMA
Drama- ngoma ni maigizo yanayoambatana na kufungamana na uchezaji wa ngoma (dansi) hadithi ya drama huigizwa kwa miondoko ya ngoma na nyimbo badala ya masimulizi na mazungumzo ya wahusika. Hii ni fani inayokubaliana sana na sanaa za maonesho za kiafrika na kwa vyovyote huweza kuwavutia na kuwasisimua watoto. Aidha hutoa nafasi kwa hadhira yenyewe kushiriki katika igizo badala ya kuwa watazamaji tu.
MICHEZO YA REDIO.
Michezo ya redio ni tamthiliya zinazotegemea sauti zaidi ya macho hivyo zinahitaji mbinu maalum za kuvutia sikio ili zifanikiwe .Hadhira huwasikiliza waigizaji wanapoongea na husikia sauti au vishindo vya mambo yanayotendeka lakini huwaoni watu hao au kuyashuhudia matukio hayo .Njia hii ya maigizo huweza kuwafikia watu wengi katika eneo kubwa.
MICHEZO YA SINEMA, RUNINGA
Hizi ni aina ya tamthiliya za kisasa zilizokusudiwa kuoneshwa katika sinema au televisheni kwa hadhira pana . Utunzi wa tamthiliya hizi unahitaji ufundi maalum, kwani uhitaji maelekezo mengi kuhusu jukwaa, mandhari, na matendo ya wahusika. Mazungumuzo ya wahusika huwa ni machache kuliko ilivyo katika mchezo wa redio au katika tamthiliya ya kawaida.
9. TAMTHILIYA GEZWA /FARAGUZI (IMPROVISED DRAMA)
Hii ni michezo inayoandaliwa bila ya kuandikwa. Waigizaji hujitungia maneno yao papo kwa papo wakati wa onesho. Njia hii hufaa sana vijijini na shuleni hupunguza sana matatizo ya ukosefu wa tamthilia zilizoandikwa. Aidha huwa hakuna lazima ya kukariri, watoto / vijana wenyewe kujitungia michezo yao na kuigiza bila ya msaada wa mtu mzima. Hii ni njia nzuri ya kupata tamthiliya nyingi za watoto na vijana. Hata hivyo tamthiliya hizi hudai ubunifu wa uwezo mkubwa wa lugha kutoka kwa waigizaji.
VIJENZI VYA TAMTHILIYA
Kwa mujibu wa kanuni za ki-Aristotle, tamthiliya yoyote kwa kawaida huwa na vipengele vifuatavyo:-
(i). hadithi (simulio) (ii) vitendo (iii) waigizaji wanaomathilisha wahusika wa hadhithi (iv) daiolojia (mazungumzo), Siku hizi daolojia yaweza kuwa ya maneno au ishara.
(i) HADITHI(SIMULIO)
Tamthiliya husimulia hadithi au kisa Fulani, Hadithi hiyo yaweza kuwa ni ya kubuni au tukio la kweli la kihistoria, au mchanganyiko wa yote mawili. Hadithi hiyo kwa kawaida kuhusu mzozo fulani unaohusisha pande mbili : upande wa mbabe (shujaa wa hadithi ) au nguli (mtendaji mkuu) na upande wa mpinzani wa mbabe/nguli. Hadithi hiyo husukwa kwa namna inayoujenga mgogoro wa pande hizo mbili hadi kufikia mwisho wake. Mtiririko wa matukio kwa kawaida huwa na umbo la piramidi lenye hatua.

HATUA ‘’A’’ CHANZO.
Katika hatua hii ndiyo huwa mwanzo au utangulizi wa mchezo. Katika hatua hii mambo yafuatayo hujitokeza:-
-Usuli wa mgogoro wa tamthiliya huelezwa .
-Hali ya tamthliya (ya majonzi, ya miujiza, ya nderemo) hudhihirishwa.
(ii) VITENDO
KITENDO
Tamthiliya hugawanyika katika sehemu kuu ziitwazo vitendo, Kila kitendo (act) huzingatia tendo kuu ndani ya mchezo, kwa mfano katika mpangilio wa matukio ulioelezwa hapo juu kila kipengele kingeweza kuwa kitendo kimoja. Hivyo tamthiliya yenye mpangilio huo kijadi ulitakiwa kuwa na vitendo vitano .katika tamthiliya ya kijunani kumalizika kwa kitendo kuliashiriwa na kuingia kwa wazumi (chorus) jukwaani. Siku hizi zipo tamthiliya zenye kitendo kimoja, vitendo viwili, vitatu, vitano, na hata zaidi.
ONESHO
Kila kitendo hugawanyika katika sehemu ndogo ziitwazo ‘’maonesho‘’, Onesho moja kwa kawaida huwasilisha tukio moja linalotendeka mahali pamoja, kwa kawaida onesho moja hutenganishwa na jingine kwa kuzingatia mantiki ya kile kinachosimuliwa, tukio moja likimalizika onesho nalo huwa linamalizika. Wakati wa maigizo, jukwaani mabadiliko ya maonesho huashiriwa kwa kufunga pazia au kuzima taa au kwa wahusika kuondoka jukwaani.
(iii). WAHUSIKA NA WAIGIZAJI
Usawiri wa wahusika wa tamhiliya hufanywa kwa njia ya matendo na mazungumzo, kwani fursa ya kutoa maelezo marefu haipo. Wahusika wa tamthiliya hawana tofauti kubwa na wahusika wa hadithi, huweza kuwa mviringo, bapa, watu wa tabaka la juu, wanyonge n.k. Tamthiliya huwa na wahusika wakuu na wahusika wadogo.
-WAHUSIKA WAKUU.
Mbabe /nguli: huyu ni shujaa wa tamthiliya ambaye matendo mengi yanahusu maisha na majaliwa yake kwa KINJEKITILE (E.Hussein 1969) ndiye mbabe au nguli (Prolagonist), yaani mhusika kiini au mtenzi mkuu.
Katika tanzia ya kijadi, mbabe aghalabu alikuwa mtu wa tabaka la juu ambaye kama tulivyokwisha elewa aliangamia kutokana na ama hila (dosari) fulani kwa tabia na maamuzi yake ama kwa sababu ya kusaka na mazingira yanayomzidi uwezo ama yote mawili wa mfalme Odipade .
Mkinzani (antagonist), Mhusika mkuu anayepambana na mbabe au nguli. Muwi (villain) mhusika muovu kwa mfano shyloak wa Shakespeare, mabepari wa venis.
-WAHUSIKA WADOGO.
Hawa aghalabu huwa ni wengi na baadhi yao huwa na jukumu dogo tu katika tamthiliya wahusika wadogo hutokea mara kwa mara ni:-
MFOILI-Mhusika anayewekwa sambamba na nguli na aliye na sifa tofauti na za nguli kwa lengo la kuwa na kumpambanua nguli vizuri zaidi.
MSIMULIZI-huyu ni mhusika anaye tumiwa na mtu kutoa maelezo na ufafanuzi kuhusu matendo na matukio katika michezo. Katika baadhi ya michezo, Katika baadhi ya michezo mhusika huyu hupewa jina jingine kama mwimba.
CHIZI (clown) -Mhusika mcheshi ambaye hufanya vitu vya kipumbavu na kusema maneno ya kijingajinga ili kuiburudisha hadhira na wakati mwingine kutoa ujumbe fulani.
WAIGIZAJI - Waigizaji pengine huitwa wamathilisha ni watu wanaotokea jukwaani mahala pa wahusika wa mchezo na kwa vitendo na tabia za hao wahusika wamahilisha .waigizaji hawana budi kuteuliwa vizuri ili wawakilishe na kuwasilisha sawa sawa umbo, hali, hisia,tabia , mawazo, na matendo ya wanaomathilisha.
(iv) DAIOLOJIA (MAZUNGUMZO YA WAHUSIKA)
Hadithi ya tamthiliya husonga mbele kwa njia ya vitendo na mazungumzo ya wahusika. Mazungumzo ya wahusika ndio huitwa daiolojia, Mafanikio ya michezo mingi hutegemea namna mtunzi anavofaulu kuweka daiolojia inayovutia na kuaminika.
Daiolojia ni lazima iwe na maneno machache yaliyoteuliwa vizuri ili kuisogeza mbele hadithi au kudhihirisha jambo fulani alilokusudia mtunzi.
Baadhi ya tamthiliya huwa na monolojia pia, Katika monolojia mhusika huzungumza mwenyewe kudhihirisha mawazo aliyonayo moyoni. Zipo pia tamthiliya zinazotumia masimulizi ambapo hutokea masimulizi na kusimulia au kusimulia mambo yaliyotokea, mithili ya mtambaji wa hadhithi au utendi, Mbinu hii hutumika katika drama tendi. Baadhi ya tamthiliya za Kiswahili kwa mfano M.Mulokozi katika MKWAWA WA UHEHE zimetumia mbinu hizi.
(v) MBINU NYINGINEZO.
Mbinu nyinginezo zinatumiwa na watunzi wa tamthiliya zimekwisha elezwa, tamthiliya za Kiswahili, hasa zile zilizoandikwa zimeiga baadhi ya mbinu za kimagharibi. Nyingi zina muundo wa ki-Arislotle zinatumia daiolojia, zina vitendo, maonyesho na migogoro inayosuluhishwa mwishoni, Baadhi ya tamthiliya zimejaribu kuiga mbinu za Sanaa za maonyesho za jadi za kiafrika. Miongoni mwa wanamajaribio hao wa mwanzo ni Ebrahim Hussein. Mtunzi huyu alijaribu kutumia mbinu za utambaji wa ngano katika maigizo yake ya NGANO ZA JADI na JOGOO KIJIJINI. Mpaka sasa wataalamu hawajakubaliana kama tungo hizo mbili ziitwe tamthiliya au tendi .
Penina Mhando pia, katika tamthiliya zake za LINA UBANI na NGUZO MAMA, vilevile alijaribu kutumia utambaji wa ngano. Mbinu ya majigambo ilitumiwa na Mhando na wenzake katika ‘’HARAKATI ZA UKOMBOZI ‘’ na Mbogo katika ‘’SUNDIATA ‘’. Mbinu ya tendi simulizi ilitumiwa na mlokozi katika mkwawa wa uhehe.

Hii ni mifano ya baadhi ya mbinu ambazo watunzi wa tamthiliya wanaweza kutumia ili kuzifanya tungo zikaribiane zaidi na utamaduni wa wale waliowaandika.

KUTUNGA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI.
Dhana ya utungaji:
Kutunga ni kitendo cha kutoa mawazo ubongoni kisha kuyadhihirisha kwa kuyaandika au kuyasimulia.

Hatua za Mwanzo za kuzingatia katika kutunga kazi za kifasihi.
i). Kuwa na jambo ambalo unaona linasababisha au lina mvuto kwa jamii.Kisha unafanyia utafiti kujua chanzo chake na kwa nini linaendelea kuwepo.
ii).Baada ya utafiti ni kufanya maamuzi ya njia gani au tanzu gani aitumie kufikisha ujumbe kati ya ushairi , hadithi, semi na maigizo.
iii).Atumie kipera gani kutoa kutoka katika tanzu aliyochagua .Mfano kama ni ushairi atumie nyimbo au ngonjera.
iv).Kulijenga jambo jambo katika fani na maudhui ili kupata mbinu sahihi ya uwasilishaji wa kazi yako kwa hadhira.
v). Mtunzi kujikita hasa katika maudhui ya jambo lako unalotaka kuliwasilisha .Mfano nini dhamira yako.
vi).Mtunzi unaangalia namna ya kuwasilisha maudhui yako, hapa unashughulikia vipengele vya fani yaani muundo , mtindo ,mandhari ,wahusika na matumizi ya lugha.
Hapa mtunzi anatakiwa atumie ufundi na ubunifu wa hali ya juu ili kazi yake ielimishe na kusisimua.
vii).Baada ya fani na maudhui kushughulilkiwa mtunzi aangalie namna ya uwasilishaji wake.Kuangalia kanuni na taratibu za kipera ulichotumia.
viii).Mtunzi unaanza kuandika yale unayotaka kuelimisha jamii kwa kufuata taratibu za uandishi.
ix). Mtunzi unasoma kuangalia kama kile ulichokidhamiria ndicho ulichikitunga.
x).Fanya mazoezi namna ya kuwaslisha hiyo kazi.
Mfano:-
Namna ya kutunga igizo la kifasihi simulizi
i.Kwanza kuteua wahusika watakao sawiri matendo ya tabia zao:-
-Mhusika mkuu hujitokeza mara kwa mara na matendo mengi yanamuhusu yeye.
-Wahusika wadogo huwa wengi.
-Kuteua waigizaji wazuri watakaofanya vizuri katika kuiwasilisha.
-Wahusika wajengwe kwa kuzingatia utendaji wao.
ii.Kuteua lugha itakayotumika.
iii.Kuteua mandhari nzuri katika uwasilishaji wake.
iv.Kuangalia muundo na mtindo wa igizo lake.

Popular posts from this blog

FASIHI KWA UJUMLA NADHARIA YA FASIHI SANAA Sanaa ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifu umbo ambalo msanii hulitumia katika kufikishia ujumbe aliokusudia kwa jamii / hadhira. AINA ZA SANAA a) Sanaa za ghibu (muziki) Inategemea na matumizi ya ala za muziki (vifaa, sauti) uzuri wa umbo la sanaa ya muziki upo katika kusikia. Sanaa hii hailazimishi fanani (msanii) na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja. Mtunzi hufanya kazi kwa wakati wake na hadhira husikiliza kwa wakati wake. b) Sanaa za ufundi Sanaa hizi hutokana na kazi za mikono. (Mfano: uchoraji, ususi, ufinyanzi, uchongaji, uhunzi, utalizi/udalizi n.k.) Mfano; - uchoraji hutegemea sana kuwepo kwa kalamu, karatasi, kitambaa, brashi, rangi n.k. uchongaji huhitaji mundu, gogo, tupa, n.k. Uzuri wa umbo na sanaa za ufundi upo katika kuona. Sanaa hii hailazimishi fanani na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja. c) Sanaa za maonesho Ni kazi mbalimbali za Sanaa ambazo hutegemea utendaji (mfa...
MAENDELEO YA KISWAHILI ASILI YA LUGHA YA KISWAHILI Neno asili lina maana kuwa jinsi kitu au jambo lilivyotokea au lilivyoanza na tunapozungumzia asili ya lugha ya Kiswahili ina maanisha tunachunguza namna lugha hiyo ilivyoanza. Wataalamu mbalimbali wa lugha wamefanya uchunguzi juu ya asili ya lugha ya Kiswahili. Uchunguzi huo umejenga nadharia mbalimbali zinazoelezea chimbuko la lugha ya Kiswahili. Kwa ujumla historia kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili ina matatizo mengi na ndiyo maana kuna nadharia mbalimbali zinazoelezea juu ya asili ya lugha ya Kiswahili. Miongoni mwa matatizo yanayoikabili historia ya Kiswahili ni pamoja na: Hakuna uthibitisho kamili juu ya nadharia zinaelezea asili ya lugha ya Kiswahili na kuenea kwake. Uchunguzi wa asili ya Kiswahili ulifanywa na wataalamu wa kizungu ambao waliandika historia ya Kiswahili jinsi walivyoelewa wao baada ya kupata ushahidi kidogo tu. Wazawa hawakushirikishwa ipasavyo katika uchunguzi wa lugha ya Kiswahili. Hapakuwa na k...
VIAMBISHI Baadhi ya watu huchanganya dhana ya viambishi na dhana ya mofimu. Lakini ukweli ni kwamba mofimu na viambishi ni dhana mbili tofauti zenye mabwiano Fulani pia. Kwa ujumla viambishi vyote ni mofimu na mofimu zote ni viambishi SWALI: VIAMBISHI NI NINI? Viambishi ni mofimu zinazoandikwa kwenye mizizi wa neno ili kukamilisha muundo wa neno husika. Katika lugha ya Kiswahili viambishi vinaweza kuandikwa kabla ya mzizi wa neno na baada ya mzizi wa neno. kwa hiyo katika lugha ya kiswahili viambishi hutokea kabla ya mzizi wa neno na baada ya mzizi wa neno AINA ZA VIAMBISHI Lugha ya Kiswahili ina viambishi vya aina mbili VIAMBISHI AWALI/TANGULIZI Hivi ni viambishi ambavyo hutokea mwanzoni mwa mzizi wa neno na huwa ni vya aina mbalimbali A.Viambishi idadi /ngeli Viambishi hivi hupatikana mwanzoni mwa majina vivumishi kwa lengo la kuonesha idadi yaani wingi na umoja, Mfano : M – cheshi wa –zuri M – tu wa - tu Ki – ti vi-ti ...
AINA ZA SENTENSI Kuna aina kuu nne za sentensi Sentensi changamano Sentensi sahili/ huru. 3. Sentensi shurutia Sentensi Ambatano 1.SENTENSI SAHILI/HURU Hii ni aina ya sentensi ambayo hutawaliwa na kishazi huru. Kishazi hicho kinaweza kuwa kifungu tenzi kimoja ambacho kinaweza kuwa na kitenzi kikuu au kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu au kitenzi kishirikishi na shamirisho Mfano: Juma ni mzembe Juma alikuwa mzembe sana Mwalimu alikuwa nafundihsa darasani MIUNDO YA SENTENSI HURU /SAHILI Muundo wa kitenzi kikuu peke yake (tawaliwa) Mfano: Wanacheza Alinipiga Wanasoma i.Muundo wa kitenzi kikuu peke yake (tawaliwa) Mfano: Wanacheza Alinipiga Wanasoma ii.Muundo wa kitenzi na kitenzi kikuu Mfano: Alikuwa anasoma Walikuwa wanataka kufundishwa ii Muundo wa kirai na kirai kitenzi Mfano; Mwalimu anafundisha Wanafunzi wanamsikiliza iii. Muundo wa virai vite...
UTUMIZI WA LUGHA Matumizi ya lugha ni namna yakutumia lugha kulingana na mila, desturi na taratibu zilizopo katika jamii husika. Ni jinsi ambavyo mzungumzaji anatunza lugha kwa kuzingatia uhusiano wake na yule anayezungumza naye. Matumizi ya lugha hutegemea mambo kadhaa Kama vile: Uhusiano baina ya wazungumzaji. -Mada inayozungumzwa -Mazingira waliyomo wazungumzaji n.k Umuhimu wa matumizi ya lugha Kuwasaidia watumiaji wa lugha kutumia lugha kwa ufasaha Kumsadia mzungumzaji kuweza kutambua kutofautiana na kutumia mitindo mbalimbali ya lugha MTINDO WA LUGHA Mtindo wa lugha ni mabadiliko yanayojitokeza katika kutumia lugha mabadiliko ya lugha katika mitindo mbalimbali yaani mitindo mbalimbali ya lugha. Kwa kawaida mtindo wa lugha / mabadiliko katika kutumia lugha ndiyo inayomwongoza mzungumzaji katika kuelewa maneno na mitindo ya tungo, Matumizi katika lugha hutawaliwa na mambo ya...
MATUMIZI YA SARUFI NADHARIA ZA SARUFI Dhana ya sarufi ya lugha imefafanuliwa na wataalamu mbalimbali wa sarufi. Mtaalamu James Salehe Mdee (1999) sarufi ya Kiswahili sekondari na vyuo anafafanua maana ya sarufi kuwa ni mfumo wa kanuni za lugha zinazomwezesha mzungumzaji kutunga sentensi sahihi na zenye kukubaliwa na wazawa wa lugha. Kanuni hizi hujitokeza katika lugha ya mzawa wa lugha inayohusika ambaye anaifahamu barabara lugha yake. Sarufi inajumuisha mfumo wa sauti maumbo ya maneno muundo na maana. Mtaalamu Mbundo Msokile (1992) na khamisi (1978) wanasema sarufi ni mfumo wa taratibu na kanuni zinazotawala matumizi sahihi ya matamshi, maumbo ya maneno, miundo ya tungo na maanda ya miundo ya lugha. Ni mfumo wa taratibu zinazomwezesha mzungumzaji wa lugha kutoa tungo sahihi na pia inamwezesha mtu yeyote anayezungumza kuelewa tungo zinazotolewa na mtu mwingine anayetuma lugha hiyo hiyo. F. Nkwera (1978) anasema sarufi ni utaratibu wa kanuni zinazomwezesha mzawa au mtumiaji ...
NOMINO /MAJINA (N) Majina ni aina ya maneno ambayo hutaja vitu, viumbe, hali au matendo ili kuviainisha na kuvitofautisha na vitu vingine. Mfano: Winnie, Werevu, Wema, Lulu, Mtu, Ubungo, Mungu na n.k AINA ZA MAJINA a.Majina ya kawaida Majina haya yanataja viumbe kama vile wanyama, miti, watu, ndege, wadudu. Majina yote hayo yanapoandikwa huanza kwa herufi ndogo kama yanatokea katikati ya sentensi au tungo. N:B Majina hayo sio maalumu kwa vitu Fulani tu bali kwa vitu mbalimbali. b. Majina ya Pekee. Haya ni majina maalumu kwa watu au mahali ambaye huonesha upekee kwa watu,mahali au vitu, Majina haya hujumuisha majina binafsi ya watu na majina ya mahali. Mfano: Marcus, Halima, James, Abel, Fredy, Anna Ubungo, Manzese, Tanzania, Uingereza, Africa N: B Majina hayo yanapoandikwa huanza kwa herufi kubwa C. Majina ya jamii. Haya ni majina ambayo yanataja vitu au watu wakiwa katika makundi au mafungu japo huwa majina hayo yapo katika hali ya umoja. Mfano,...
KUBAINISHA MOFIMU Kubainisha mofimu ni kuligawa neno katika mofimu zinazolijenga neno na kueleza kazi za kila mofimu ubabaishaji huo wa mofimu hufuata hatua zifuatazo 1. Kutambua aina ya neno – Yaani kama neno hilo ni tegemezi au neno changamano, Neno huru huundwa na mofimu huru na neno tegemezi huundwa na mofimu tegemezi na neno changamano huundwa na moja huru na mengine tegemezi N: B Neno huru huwa halivunjwi vunjwi kwani huundwa na mofimu huru 2. Kulitenga neno na kulivunja vunja katika mofimu zinazojenga neno hilo yaani hujenga mofimu awali, mzizi na mofimu tamati. N: B Mofimu awali, mzizi na mofimu tamati hupatikana katika maneno tegemezi na maneno changamano 3. Kueleza kazi ya kila mofimu Mfano: Bainisha mofimu katika maneno yafuatayo Hatukupendi Hili ni neno tegemezi ii. 1- Mofimu awali kianzishi, nafsi ya kwanza wingi 2 - Mofimu awali rejeshi kwa mtendwa 3 - Mofimu awali rejeshi kwa mtenda 4 - Mofimu mzizi 5 ...
UTUNGAJI Maana ya utungaji Utungaji ni pato la akili ya mtu binafsi ambayo hurejeshwa kwa fani kama vile macho, ushairi, tamthiliya au hadithi. Utungaji ni kitendo cha kuyatoa mawazo ubongoni, kuyakusanya na kisha kuyadhihirisha kwa kuyaandika au kuyazungumza. Ni kitendo cha kuunda hoja na kuyapanga katika mtiririko unaofaa katika lugha kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii husika. SIFA ZA MTUNGAJI Mtunzi analazimika kuelewa kikamilifu mada inayoshughulikiwa. Mtungaji lazima azingatie kanuni na taratibu za uandishi. Mtungaji anatakiwa kuzingatia mpango mzuri na wenye mantiki wa mawazo kutoka mwanzoni hadi mwishoni. Mtungaji anapaswa kuwa na msamiati wa kutosha ili kumwezesha kutumia lugha bora, sanifu, na fasaha. Mtunzi anapaswa kuzingatia sarufi ya lugha anayoitumia. Mtunzi anapaswa kujali nyakati zinazofaa. Mtunzi anapaswa kuwa na uwezo wa kutosha wa kuhusisha yanayoelezwa na hali halisi ilivyo katika j...