Skip to main content




UTUMIZI WA LUGHA


Matumizi ya lugha ni namna yakutumia lugha kulingana na mila, desturi na taratibu zilizopo katika jamii husika. Ni jinsi ambavyo mzungumzaji anatunza lugha kwa kuzingatia uhusiano wake na yule anayezungumza naye. Matumizi ya lugha hutegemea mambo kadhaa Kama vile: Uhusiano baina ya wazungumzaji.
-Mada inayozungumzwa
-Mazingira waliyomo wazungumzaji n.k
Umuhimu wa matumizi ya lugha
Kuwasaidia watumiaji wa lugha kutumia lugha kwa ufasaha
Kumsadia mzungumzaji kuweza kutambua kutofautiana na kutumia mitindo mbalimbali ya lugha
MTINDO WA LUGHA
Mtindo wa lugha ni mabadiliko yanayojitokeza katika kutumia lugha mabadiliko ya lugha katika mitindo mbalimbali yaani mitindo mbalimbali ya lugha. Kwa kawaida mtindo wa lugha / mabadiliko katika kutumia lugha ndiyo inayomwongoza mzungumzaji katika kuelewa maneno na mitindo ya tungo,
Matumizi katika lugha hutawaliwa na mambo yafuatayo.
Uhusiano baina ya wazungumzaji
Mada ya mazungumzo
Lengo au madhumuni ya mazungumzo
Sifa za wazungumzaji
Jinsi mazungumzo yanavyofanywa
Utanzu wa mawasiliano
A.Mazingira /muktadha
Ni wazi kwamba wazungumzaji huzungumza wakiwa katika mazingira Fulani yanayotawala katika maisha yao ya kila siku. Mazingira hayo yanaweza yakawa ya hotelini shuleni, ofisini, mahakamani na n.k
B.Uhusiano baina ya wahusika
Uhusiano baina ya wahusika huathiri mtindo wa uzungumzaji katika lugha. Mzungumzaji atatumia lugha kwa kutegemea anaongea na nani na kutokana na sababu hiyo tunapata lugha ya baba na mtoto, watu wa rika moja, mtu na mpenzi wake, mtu na mwanafunzi wake mfanyakazi wa kawaida na mkuu wake wa kazi na n.k.
C.Mada ya mazungumzo
Kimsingi mada ya mazungumzo hutawala usemaji na namna ya uzungumzaji kwa ujumla na kutokana na mada ya mazungumzo tunapata lugha ya kibiashara, kitaalamu, kitabibu, kitaaluma na kisiasa na n.k
D.Madhumuni ya mazungumzo
Wakati mwingine mitindo wa lugha hutawaliwa na madhumuni ya mazungumzo na kutokana na madhumuni ya mazungumzo uzungumzaji utategemea mazingira, uhusiano baina ya wahusika pamoja na mada ya mazungumzo.
E. Jinsi mazungumzo/mawasiliano yanavyozungumzwa
Namna mawasiliano yanavyofanyiwa inaweza kuathiri mtindo wa uzungumzaji. Mawasiliano yanawezakufanywa kwa njia ya maandishi au mazungumzo ya mdomo yanaweza kufanyiwa kwa njia ya simu au televisheni au redio. Njia hizi huathiri mtindo wa uzungumzaji.
F. Utanzu wa mawasiliano
Mtindo wa uzungumzaji unaweza kuathiriwa pia na utanzu wa mawasiliano yaani kama ni hotuba, majadiliano masimulizi, mazungumzo ya kawaida au maelezo, vitathiri mtindo wa uzungumzaji
Sifa ya mzungumzaji
Wakati mwingine mtindo wa lugha huathiriwa na sifa za wazungumzaji, Sifa hizo zaweza kuwa; kiwango cha elimu, cheo, uwezo wa kipato, heshima ya mtu katika jamii na n.k

I. Rejesta
Ni mtindo wa lugha ambayo hutumika mahali penye shughuli fulani, mf: bandarini, shuleni, hospitali, hotelini, kanisani nk.

AINA ZA REJESTA
Kuna aina mbalimbali za rejesta kulingana na mahali au shughuli inapofanyika.
i. Rejesta za hotelini:- huu ni mtindo utumikao hotelini mf:- Nani wali kuku? Chai moja chapati moja
ii.Rejesta za mitaani:- ni mazungumzo yatumiwayo na aina fulani ya watu katika magenge, vijiweni na hueleweka na watu au wahusika wenyewe. Mf: mshikaji-rafiki, Demu-msichana, umenoa- umekosa, dili maiti -mpango usiofanikiwa.
iii.Rejesta za hospitalini:- ni lugha itumiwayo na manesi, madaktari na wagonjwa hospitali. Lengo lake ni kupunguza muda kuwashughulikia wateja wengi. mf: kutwa mara tatu yaani kunywa kimoja asubuhi, mchana na jioni.
iv.Rejesta kanisani:- ni lugha ya mahubiri. Sifa yake kubwa haibadiliki badiliki. mf: Mapendo - daima, Bwana yesu asifiwe - Amina.
Msikitini, mf: Asalam aleikum - Aleikum asalaam
v.Rejesta mahakamani:- mtindo huu hutumika mahakamani. Mf: Mheshimiwa hakimu, Mtuhumiwa, kesi nk.

DHIMA ZA REJESTA
i. Hutumika kama kitambulisho kwa wazungumzaji, mtu huweza kutambua shughuli baada ya kusikia lugha itumikayo, mtindo wa sokoni ni tofauti na mahakamani hivyo hutambulisha wazungumzaji.
ii. Hutumika kurahisisha mawasiliano kwa kupunguza muda wa kuhudumia, mf: Hotelini kama wateja wengi, Nani wali samaki?, Chai wapi?
iii. Hukuza lugha, msamiati wa lugha huongezeka kupitia rejesta mf: dawa mpya - ikimaanisha dawa za kupunguza makali ya ukimwi.
iv. Huficha jambo kwa wasiohusika, mf: daktari amuandikiapo majibu mgonjwa sio rahisi mtu asiye katika kada hiyo kuelewa.
Mf: BS - kupima malaria
Stool - kupima choo
Inj - Sindano
5/7 - kunywa dawa kwa siku 5 katika wiki
v. Hupamba lugha, mikato ya maneno katika rejesta, inapamba lugha. mf: wali kuku, wapi mkia
vi. Hutumika kupunguza ukali wa maneno mf: kujifungua - kuzaa
II. MISIMU (SIMU)
Misimu ni maneno yanayounda na kutumiwa na watu kwa muda fulani na baadaye kupotea. Misimu ni maneno yasiyokuwa sanifu yanayozushwa na kikundi cha watu wachache wenye utamaduni mmoja ili kuelezea mahusiano yao kama kikundi na hatimaye maneno yale hutumiwa na watu kwa muda fulani yale yanayodumu husanifiwa na kuwa sehemu ya msamiati rasmi katika luha husika.
Misimu husuka na kutoweka ingawa baadhi ya misimu inaweza ikatumika kwa muda mrefu na kusanifiwa kuwa lugha rasmi.
Misimu hutumiwa na makundi maalum katika jamii, yaliyojitenga kufuatana na mambo yanayoendelea, mazoezi, kazi au shughuli.
CHANZO CHA MISIMU
Misimu huzuka kutokana na mabadiliko na matukio mbalimbali yanayojitoleza katika jamii kama vile hali ngumu ya maisha, mabadiliko ya tabia za watu.
Baadhi ya misimu huzuka kutokana na hali ya utani miongoni mwa watu mbalimbali kwa lengo la kukebehi, kubeza, kudharau, kudhihaki, kukejeli au kusifia kusiko kuwa kwa kawaida.
SABABU ZA KUTUMIA MISIMU
Kutaka kuyafanya mazungumzo yawe ya siri. Kuna baadhi ya watu wanapozungumza ili kuyafanya mazungumzo yao yasieleweke kwa watu wengine hutunza misimu ili kuyafanya mazungumzo yao yawe ya siri.
Baadhi huitimiza kwa kudhani matumizi ya misimu ndiyo ujuzi wa lugha. Hali hii hujitokeza hasa kwa vijana ambao hupenda kutumia misimu kama sifa mojawapo ya kuonesha ujana wao. Ni vigumu kuwasikia wazee wa makamo tena wenye heshima zao wakitumia misimu.
Kufanya mambo mazito na ya maana yaonekane mepesi na ya kawaida.

AINA ZA MISIMU
Misimu inaweza ikagawanywa katika makundi mbalimbali kwa kutumia vigezo tofauti:-
(a) MADA
(i) Misimu inayohusiana na pesa. Upungufu wa pesa madeni, rushwa, utajiri na mambo yanayowakumba watu katika jamii. Ili kuelezea hali hizo watu wamezusha misimu kama vile kuchacha, kupigika, kufulia, pedeshee, kumkamua mtu, kuchuna.
(ii)Misimu inayohusika na vyakula. Kwa kawaida misimu hii husifu chakula kilicho kizuri na kitamu, cha watoto – wali, wali mchafu, -pilau, kodrai ukoko, zege – chipsi mayai , kiepe – chipsi.
iii Misimu ya ulevini. Hii hutumika katika mazingira ya ulevi ili kuyafanya mazingira hayo yawe ya msisimko na yenye starehe kwa walevi.
Mfano: Leta kama tulivyo
-Moja baridi, moja moto
-Leta kisichana
-Kupiga mtindi
(iii) Misimu ya nguo. Uvaaji wa nguo na mitindo mbalimbali ya nguo imezalisha misimu kama vile:-
Mfano: pedo
Kitopu
Mnyonyo
Kibamba
Tentemeke
Wanchoma kumoyo
Mayenu
Kutupia
(iv) Usafiri: - Hii hutumika mahali penye shughuli za usafiri.
Mfano: daladala
Vipanya
Bodaboda
Pipa – ndege
Gogo
(b) MAKUNDI YA WATU-
Kwa kutumia kigezo hiki misimu kinaweza kugawanywa katika makundi yafuatayo:-
(i) Misimu ya wanafunzi
(ii) Misimu ya wafanyabiashara
(iii) Misimu ya majangili
(iv) Misimu ya majambazi
(v) Misimu ya wanamichezo
(vi) Misimu ya mafundi
(vii) Misimu ya wanawake.
(c) Kwa kutumia kigezo cha kawaida kuna misimu hii.
(i) Misimu ya pekee, ambayo huelezea mahusiano ya kikundi kimoja kutoka katika utamaduni mmoja. Misimu hii hupatikana sehemu moja ya kazi au mahali waishipo watu wa aina moja. Misimu hii kimatumizi eneo lake huwa ni dogo na inaitwa misimu ya pekee kwa sababu haijulikani zaidi nje ya eneo ilimozuka na kutumika.
(ii) Misimu ya kitarafa ambayo eneo lake kimatumizi ni kubwa kidogo kulingana na lile la misimu ya kipekee
Misimu hii inaweza ikapatikana katika kata, tarafa, wilaya , mkoa. Watu waliopo katika kundi hili wanamchanganyiko wa utamaduni na si rahisi kutambua mipaka ya maeneo haya ya kitarafa ingawa kimsingi yanaweza kuwa ya kijografia kilugha. Kuenea kwa misimu hii kunategemea hali au tabia ya kuingiliana kwa watu katika shughuli zao za kila siku kama vile kuoana n.k. Mara nyingi hutokana na vitu vilivyo katika sehemu husika, lugha itumikayo uzoefu wa mazingira na uwezo wa lugha wa wahusika (umahiri)
(iii) Misimu zagao
Hii ni misimu ambayo imeenea nchi nzima na wakati mwingine kuvuka mipaka ya nchi, Hutumika katika radio, televisheni, magazeti lakini pia hutumika katika baadhi ya vitabu. Inapotumika kwa muda mrefu huweza kusanifiwa na kuwa msamiati rasmi.
Mfano: buzi, changudoa, wafurukutwa, kuchakachua , ngangari , mafataki, Serengeti boy, nyumba ndogo, kuchuna, daladala, shangingi, dingi, mshua, mahanjumati, mkorogo.
MATUMIZI YA MISIMU
Misimu hutumika kama kiungo cha ukuzaji wa lugha. Baadhi ya misimu hasa ile inayodumu kwa muda mrefu huweza kusanifiwa na kuwa sehemu ya lugha rasmi. Mfano: marupurupu, chungu mbovu, magendo, daladala, mitumba, changudoa.
Kupamba lugha hasa katika maongezi na katika maandishi hasa katika fasihi. Matumizi ya misimu katika kuipamba lugha huifanya lugha isisimke na kufurahisha.
Kufanya mawasiliano yawe mafupi na yanayoelezwa kwa haraka. Misimu
inawezesha watu kuwasiliana kwa kutumia maneno machache na muda mchache. Mfano: daladala
Kuficha lugha ya matusi. Baadhi ya misimu hutumika kupunguza ukali wa maneno katika mazungumzo ya kawaida. Mfano: mada inayohusiana na mapenzi misimu hutumika sana ili kupunguza ukali wa maneno hayo. Kula – uroda.
Kuunganisha watu wa makundi mbalimbali. Mfano:- makundi ya maprofesa, wanasheria, wasomi, madaktari wanapotumia misimu huwekwa katika kundi moja.
Kuhifadhi historia ya jamii. Kwa kuwa misimu huzuka na kutoweka kutokana na mabadiliko yanayojitokeza katika jamii, mara nyingi misimu hiyo hutumika kuonesha historia ya jamii husika.
Mfano: bwanyenye wapambe
Ukupe wazawa
Ubeberu ngangari
Utaifishaji ngunguri
Ukereketwa
Mfurukuwa
Kuibua hisia mbalimbali:- Misimu huwa na maneno yenye kubeba hisia za chuki, furaha, huzuni, kejeli n.k
Misimu inafurahisha na kuchekesha. Kwa kuwa hazina chumvi nyingi na hivyo kufurahisha na kuchekesha.
Kukosoa na kuiasa jamii kwa kuwa hubeba hisia za kebehi, dhihaka,, chuki, kejeli, mabezo, dharau na kusifu kusikokuwa kwa kawaida.
MATATIZO YA MISIMU
Misimu siyo lugha sanifu kwa hiyo kwa namna moja au nyingine huchangia kuharibu lugha.
Misimu hupunguza hadhira ya watumiaji wa lugha fulani.
Misimu huzuka na kutoweka, Misimu iliyozuka na kutoweka ni mingi zaidi ukilinganisha na ile iliyodumu na kuingizwa katika msamiati rasmi hivyo mchango wake katika kukuza ni mdogo.
Misimu ina maana nyingi, Maana hizi huweza kuwepo,
Misimu huwa na chuku nyingi. Hali hii husababisha misimu kutokuaminika katika jamii na hivyo kusababisha mawasiliano kutenguka.
Misimu ni lugha ya mafumbo.Kutokana na hali hii misimu hufahamika na watu wanaoitumia na hivyo kusababisha mawasiliano kuwa kidogo.
NB: Nafasi ya misimu katika kuikuza lugha ya Kiswahili na kubwa kwa sababu matumizi ya misimu yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku na imekuwa ikitumika katika mazungumzo ya kawaida na hata katika maandishi. Kwa kiasi kikubwa kuenea kwa misimu kumesababishwa na vyombo vya habari kama vile magazeti, televisheni. Kwa upande wa magazeti misimu imeenezwa sana na magazeti ya udaku. Pia vipindi mbalimbali katika televisheni na redio vimekuwa vikichangia kuenea kwa kasi kwa misimu hii, matokeo yake ni kwamba baadhi ya misimu imepata nguvu na kushamiri na mengine imevuka mipaka ya nchi. Hali hii imechangiwa na matumizi ya mara kwa mara ya misimu hiyo katika kutolea habari. Kutokana na hali hii hata kamusi za Kiswahili zilizotengenezwa hivi karibuni zimejumuisha baadhi ya misimu kama misamiati inayomchango katika kuikwea lugha ya Kiswahili.
Swali:- Lugha izungumzwapo mitaani na vijana huchukiwa sana na wazazi lakini wasanifu wa lugha wanaipenda sana lugha hiyo. Toa sababu za mkungazo wa mawazo kati ya wazazi na wasanifu wa lugha.



III. UMAHIRI WA LUGHA
Umahiri katika lugha ni ujuzi wa kiwango cha juu katika lugha fulani ambao hukita katika stadi nne za lugha yaani kusoma, kuzungumza, kuandika na kusikia.
Umahiri unaweza kugawanyika katika makundi makuu mawili
(i) Umahiri katika lugha
(ii) Umahiri wa lugha
UMAHIRI KATIKA LUGHA
Umahiri katika lugha ni ujuzi wa kiwango cha juu katika lugha fulani kwa viwango vyote vya lugha yaani kuzungumza, kusikia, kusoma na kuandika.
Aidha umahiri katika lugha huhusiana na ujuzi wa hali ya juu katika lugha moja tu.
Mfano, Kiswahili peke yake, kiingereza peke yake au lugha za kilugha peke yake
II UMAHIRI WA LUGHA
Umahiri wa lugha ni ujuzi wa hali ya juu wa lugha zaidi ya moja katika staidi zake zote yaani kuzungumza, kusikia, kusoma na kuandika. Umahiri wa lugha unahusu ujuzi wa lugha zaidi ya moja. Mfano, Kiswahili na lugha za kikabila, Kiswahili na kiingereza. Mtu mwenye ujuzi wa umahiri huitwa mmahiri, katika nchi yetu kundi kubwa la watu ni wamahiri, wanafahamu lugha zao za kikabila, na Kiswahili na hata lugha za kigeni.
SABABU ZINAZOSABABISHA UMAHIRI
Umahiri kusababishwa na mambo kadhaa:-
Elimu
Mtu anaweza akawa mahiri wa lugha katika kusomea lugha husika au kuitunza lugha husika anapokuwa anasoma. Elimu humwezesha mtu kupata ujuzi wa msamiati, matamshi yake, sarufi, maana na mbinu nyingine za lugha hiyo. Mambo haya humwezesha mtu kuwa mahiri katika lugha au mahiri wa lugha.
Matumizi ya lugha ya kila siku:-
Matumizi ya kila siku humwezesha mtu kuwa mahiri na hii hutegemea lini wakati gani, mara ngapi, na kwa kiwango gani mtu huitimiza lugha hiyo katika shughuli zake za kila siku kama vile mawasiliano, sherehe n.k
Hamahama ya watu kutokana na sababu mbalimbali kama vile vita, ajira, biashara dini n.k
Mabadiliko katika sera ya lugha:-
Maamuzi yanayofanywa na serikali katika matumizi ya lugha yanaweza kusababisha mtu kuwa mmahiri wa lugha. Mfano: kama serikali itaamua kufuta katika matumizi ya lugha ya Kiswahili kuhimiza matumizi ya lugha za kigeni kama vile kiingereza na kifaransa ni wazi kuwa watu watalazimika kujifunza lugha hizo na hivyo kuwa wamahiri wa lugha hizo.
ATHARI ZA UMAHIRI
Watu wengi katika nchi yetu ni wamahiri wa lugha kwamba wengi wanazungumza lugha zao mama pamoja na za kigeni kama vile kiarabu, kihindi, kifaranza n.k
Kutokana na kuzungumza lugha zaidi ya moja huwa kunakuwa na mwingiliano wa lugha hizo unajitolea katika matamshi, msamiati, miundo na maana.
I. MATAMSHI:-
Kwa kawaida matamshi ndiyo humbainisha mzungumzaji kuwa lugha yake ya kwanza ni ipi. Watanzania wengi waliozaliwa vijijini huanza kujifunza lugha za kikabila kabla ya Kiswahili na wale waliozaliwa mjini hujifunza lugha ya Kiswahili na baadaye lugha nyingine za kigeni au za kikabila.
Mambo haya hupelekea athari ya lugha ya kwanza kujitokeza unapozungumza lugha ya pili. Kwa mfano Wakurya wanapozungumza hushindwa kutofautisha herufi ya ‘r’ na ‘l. Wanyakyusa huchanganya kati ya herufi ‘f’ na ‘v’. Wamakonde kuchanganya ‘n’ na ‘m’. Kuongeza vitamkwa baadhi ya wazungumzaji ambao wazungumzapo Kiswahili huongeza vitamkwa kutokana na kuathiriwa na lugha zao mama. Mfano; Nakwendaga, hakunaga – hutumiwa sana na wasukuma, Bukubwa badala mkubwa, Ndada badala ya dada
II. MSAMIATI
Baadhi ya wazungumzaji wanapozungumza huchanganya misamiati, Mfano msamiati wa kiingereza na Kiswahili au Kiswahili na lugha za kikabila.
III. MIUNDO
Wakati mwingine muundo wa lugha ya kwanza hujitokeza mtu anapozungumza lugha ya pili. Mfano: Mama Kaondoka mjini. Wanyamwezi wamakua, wamatengo unapozungumza na mtu unayemweshimu sana unatumia wingi badala ya umoja.
IV. MAANA
Mara nyingi mahiri wa lugha huonesha athari katika maana anapokuwa anazungumza.
Mfano: Kuna baadhi ya watu wanapozungumza, maana za maneno za lugha fulani wanazozumgumza hujitokeza katika lugha nyingine.
Wangoni hutumia neno kuchacha wakimaanisha kuwa kichachu, kichungu, kikali na ukakasi. Ni wazi kuwa wangoni wananeno moja tu katika lugha yao ambalo kubeba maana hizi zote.
Wanyamwezi wanapozungumza Kiswahili hawawezi kutofautisha neno jana na kesho kutwa kutokana na sababu kuwa katika lugha yao wana neno moja tu ambalo huwa na maana zote mbili za neno hilo ni ‘igolo’
LUGHA YA MAZUNGUMZO NA LUGHA YA MAANDISHI:-
Kwa ujumla lugha huwa ni moja yaani lugha ya mazungumzo tu. Lakini kutokana na namna lugha inayowasilishwa inaweza kugawanywa katika makundi makuu mawili:-
(i) Lugha inayowasilishwa kwa njia ya maandishi ya mdomo / lugha ya mazungumzo.
(ii) Lugha inayowasilishwa kwa njia ya maandishi (lugha ya maandishi).
LUGHA YA MAZUNGUMZO:-
Hii ni lugha inayowasilishwa kwa njia ya mazungumzo ya mdomo. Chanzo chake ni kuzungumza mawasiliano kati ya chanzo / mzungumzaji na kikomo /msikilizaji ni lazima wawe na sifa mahususi.
SIFA ZA MZUNGUMZAJI
Inatakiwa azingatie ufasaha na usanifu wa lugha.
Azingatie mpango mzuri wa mawazo.
Awe muwazi na mkweli katika maelezo yake.
Asiwe na hitilafu katika viungo vinavyotumika kuzungumza na kusikiliza.
SIFA ZA MSIKILIZAJI:-
Anatakiwa awe mtulivu na msikivu. Pia inategemea viungo vya mwili.
Aweze kufahamu yanayozungumzwa.
Aweze kutafsiri yanayozungumzwa.
Aweze kupima yale aliyoyasikia na uzoefu wake wa siku zote.
LUGHA YA MAANDISHI
Hii ni lugha inayomwezesha mtu kujieleza kwa njia ya maandishi. Chanzo chake ni kuandika na kikomo chake ni kusoma. Ili mawasiliano yaweze kuwepo kati ya mwandishi na msomaji ni lazima kanuni za uandishi zizingatiwe na mwandishi na msomaji afahamu kusoma.
TOFAUTI KATI YA LUGHA YA MAZUNGUMZO NA
LUGHA YA MAANDISHI
Lugha ya mazungumzo na ya maandishi zinatofauti kadhaa:-
1. UWASILISHAJI
Lugha ya mazungumzo huwasilishwa kwa mazungumzo ya mdomo, kwa sauti. Lakini lugha ya maandishi huwasilishwa kwa njia ya maandishi au kwa njia ya kuandika.
2. CHANZO NA KIKOMO:-
Chanzo cha lugha ya mazungumzo ni kuzungumza yaani mzungumzaji na kikomo chake ni kusikiliza yaani msikilizaji. Lakini chanzo cha lugha ya maandishi ni kuandika yaani mwandishi na kikomo chake ni kusoma .
UHUSIANO NA HADHIRA
Lugha ya mazungumzo huwakutanisha ana kwa ana mzungumzaji na msikilizaji. Lakini lugha ya maandishi mara nyingi haiwakutanishi ana kwa ana mwandishi na msomaji.
MABADILIKO
Lugha ya mazungumzo hubadilika badilika kutokana na mazingira, mahusiano baina ya watu wanaozungumza, pamoja na wakati na hapo tunaweza kupata rejesta mbalimbali. Lakini lugha ya maandishi ikishaandikwa haibadiliki kutokana na mazingira, wahusika wala wakati.
UHAI
Lugha ya mazungumzo huwa ni hai zaidi kuliko lugha ya maandishi kwa sababu huonesha hali ya mzungumzaji kama vile furaha, huzuni, chuki au hasira . Lakini lugha ya maandishi haioneshi wazi hisia.
Lugha ya mazungumzo humweka mtu huru zaidi na hapo tunaweza tukapata
umahiri wa lugha ya mzungumzaji kama vile matumizi ya misimu, semi, athari za lugha yake ya kwanza, kiimbo n.k. Lakini lugha ya maandishi huzingatia zaidi usanifu wa lugha.
GHARAMA
Lugha ya mazungumzo haina gharama kubwa kwa sababu hutumia viungo vya mwili. Lakini lugha ya maandishi inagharama kubwa katika muda wa kuandika na vifaa vingine kama kalamu, karatasi n.k
8. UHIFADHI
Lugha ya mazungumzo ni vigumu kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadaye ikiwa vile vile kama ilizungumzwa lakini lugha ya maandishi ni rahisi kuhifadhiwa na hudumu kwa muda mrefu kwa matumizi ya baadaye.
9. Lugha ya mazungumzo huonesha shada, kiimbo, na lafudhi si rahisi kubaini mambo yao.
10. WAHUSIKA
Lugha ya mazungumzo inawahusika wengi kuanzia watoto hadi watu wazima, vichaa na wenye akili timamu. Lakini lugha ya maandishi wahusika wake ni wachache, yaani wanaojua kusoma na kuandika tu.
KUFANANA KWA LUGHA YA MAZUNGUMZO NA LUGHA YA MAANDISHI
Lugha zote hizi mbili humuhusu mwanadamu.
Lugha zote mbili hutumiwa na mwanadamu kwa lengo la kukidhi haja ya mawasiliano.
Lugha zote mbili huwa na chanzo na kikomo.
Lugha zote hutumiwa kama alama ya utambulisho wa jamii fulani.
Zote huwa zinahitaji maandishi ingawa mwandalizi ya lugha ya mazungumzo huwa ni kidogo sana.
MAKOSA YA KISARUFI NA MAKOSA YA KIMANTIKI KATIKA
LUGHA YA KISARUFI
Haya ni makosa yanayotokana na kukiukwa kwa taratibu za kisarufi yaani matamshi ya maneno, miundo ya tungo, miundo ya maneno na maana za maneno. Mara nyingi makosa haya hutokana na utumiaji mbaya wa lugha miongoni mwa wazungumzaji. Kwa ujumla makosa ya kisarufi yanaweza kugawanyika katika makundi yafuatayo:-
Makosa ya matamshi:- Makosa hayo hujitokeza watu wanapozungumza kwa kushindwa kutamka baadhi ya sauti za Kiswahili au kuzichanganya na wakati mwingine ….
Mfano:- Kuna baadhi ya watu huchanganya ‘r’ na ‘l.’
- Naenda kurara
Wengine wanatumia‘s’ badala ya ‘z’, ‘dh’ na ‘Hi’
- Sahabu badala ya dhahabu
- Samani sile badala ya zamani zile
- Sambi badala ya dhambi.
- Dhibiti badala ya thibiti
- Anapashwa badala ya paswa.
Kwa kawaida makosa haya hutokana na athari ya lugha ya kwanza.
Kuongeza vitamkwa:-
Makosa haya hufanya na wazungumzaji wanapokuwa wanazungumza kwa kuongeza vitamkwa katika maneno ambayo huwa havihitajiki katika maneno hayo na hivyo kuiharibu lugha hiyo.
Mfano: Tunakwendaga kwao mara kwa mara.
Hakunaga kitu kama hicho.
Yule mbaba jamani!
Kosa la kuacha maneno:-
Wazungumzaji baadhi wanapozungumza Kiswahili huacha maneno fulani katika sentensi na bado wakifikiri wanatoa ujumbe ulio kamili.
Mfano: - Mama ameondoka mjini
Mama ameenda mjini.
- Baba yako amerudi kazini?
Baba amerudi kutoka kazini?
Kosa la tafsiri sisisi:-
Makosa yanatokana na tafsiri moja kwa moja na hivyo kusababisha makosa ya kisarufi katika lugha.
Mfano: aidha …….au
Mama aidha atakuwa mjini au kazini.
Osha uso wako badala ya nawa uso wako.
Makosa ya kimuundo:-
Makosa yanayojitokeza katika muundo, kwa kawaida miundo ya lugha ya Kiswahili huanza na nomino ya mtenda au mtendwa na kufuatwa na jambo analotendwa au analotenda yaani vitenzi.
Mfano: Sikuwa ninajua kuwa Grace ni dada yako
Sikujua kuwa Grace ni dada yako.
MAKOSA YA KIMANTIKI
Mantiki ni utaratibu mzuri wa kufikiri. Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu toleo la pili (2004) inafasili mantiki kuwa ni mtiririko wa fikra zilizopangwa ili kujenga hoja yenye kukubalika. Kutokana na fasihi hizi makosa ya kimantiki ni yake yanayoonesha kukosekana kwa utaratibu mzuri wa fikra au makosa yanayotokana na upotofu wa mawazo ya mzungumzaji. Kwa maneno mengine ni makosayanayotokana na kukosekana kwa mtiririko mzuri wa fikra zilizopangwa ili kujenga hoja zenye kukubadilika.Kwa kawaida wazungumzaji na waandishi hufanya makosa ya kimantiki.
Mfano: Nyumba yangu imeingia siafu
Nyumba haiwezi kuingia siafubali siafu huingia ndani ya nyumba
- Siafu wameingia ndani ya nyumba yangu.
- Gari yangu imeibiwa
- Gari ndiyo imetedwa
- Gari yangu imeibwa
NB: Makosa ya kisarufi nay a kimantiki ni ya kawaida ambayo yapo na yataendelea kuwepo katika lugha. Jambo la msingi ni kuendelea kujazwa kabisa yasitumike katika taasisi rasmi kama vile shule barua rasmi na madhara na mikutano ya kitaaluma n.k Ni vizuri katika kutekeleza azima hii ya kuzuia makosa ya kimantiki na kisarufi mkazo wa marekebisho …. Tangu kiwango cha awali,
Hii itasaidia kupunguza makkosa hayo kwa siku za baadaye. Kwa upande mwingine makosa haya husambazwa na vyombo vya habari na baadhi ya waalimu. Kwa hiyo ni vizuri walimu pamoja na vyombo vya habari kusisitiza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.
UTATA KATIKA MATUMIZI YA LUGHA
Utata ni nini?
Utata ni kitendo cha tungo kuwa na maana zaidi ya moja au kueleweka kwa namna mbili zaidi tofauti. Mara nyingi utata hujitokeza katika maana za maneno au maana za sentensi.
SABABU ZINAZOSABABISHA UTATA
Matumizi ya maneno yenye maana zaidi ya moja bila kuyapa muktadha wa kimatumizi.
Mfano: Mama ana mbuzi
Neno mbuzi lina maana mbili na hivyo hufanya sentensi zieleweke kuwa na namna mbili tofauti.
Kutozingatiwa kwa taratibu za uandishi.
Mfano: Nilimkuta Juma na rafiki yake George
-Mama John amekuja
Katika lugha ya mazunguzo utata unaweza ukasababishwa na kutokuweka mkazo wa sauti mahali panapostahili katika neno.
Mfano: - Mbuzi
- Mbuni
- Mbuni
Utata unaweza ukasababishwa na matumizi ya mashina lugha ya picha au lugha ya mtaani au lugha iliyojificha.
Mfano: Juma anaua chumbani mwake
- anatoa uhai
- Ana msichana mzuri chumbani mwake
- Ana maua chumbani mwake


NAMNA YA KUONDOA UTATA
Kuyapa maktadha wa kimatumizi maneno yenye maana zaidi ya moja.
Mfano: Mama ana mbuzi wengi
Mama ana mbuzi ya kukuna nazi.
Kuweka mkazo wa sauti katika silabi stahiki katika neno.
Mfano: Mbuni - Mbuni ni mzuri
Mbuni – Mbuni ni mzuri
Utata unaweza ukaondolewa kwa kuzingatia matumizi sahihi ya alama za uandishi.
Mfano: Baba, John amefika
Baba John, amefika
Kuepuka matumizi ya lugha ya picha.
Mfano: Juma anaua chumbani mwake
- Mzungumzaji aliyetumia sentensi hii akiwa anakusudia kuonesha kuwa Juma ana mchumba mzuri nyumbani kwake alipaswa kuepuka matumizi ya picha kwa kusema “Juma ana mchumba mzuri nyumbani kwake” Kwa kufanya hivyo angekuwa ameondoa utata uliokuwepo katika sentensi ya awali
NB: Wakati mwingine utata unaweza ukasababishwa na matumizi ya kutanguliza nomino ya mtendwa badala ya kutangulia nomino ya mtenda.
Mfano: Simba ameuawa na askari pori
- Sentensi hii ni tata kwa sababu ina maana zaidi ya moja.
(i) Simba na askari pori wote wameuawa.
(ii) Askari ndiye aliyemuua samba
Kama nomino ya mtenda ingetangulia kusingegkuwa na utata.

- Askari pori ameua simba.

Popular posts from this blog

FASIHI KWA UJUMLA NADHARIA YA FASIHI SANAA Sanaa ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifu umbo ambalo msanii hulitumia katika kufikishia ujumbe aliokusudia kwa jamii / hadhira. AINA ZA SANAA a) Sanaa za ghibu (muziki) Inategemea na matumizi ya ala za muziki (vifaa, sauti) uzuri wa umbo la sanaa ya muziki upo katika kusikia. Sanaa hii hailazimishi fanani (msanii) na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja. Mtunzi hufanya kazi kwa wakati wake na hadhira husikiliza kwa wakati wake. b) Sanaa za ufundi Sanaa hizi hutokana na kazi za mikono. (Mfano: uchoraji, ususi, ufinyanzi, uchongaji, uhunzi, utalizi/udalizi n.k.) Mfano; - uchoraji hutegemea sana kuwepo kwa kalamu, karatasi, kitambaa, brashi, rangi n.k. uchongaji huhitaji mundu, gogo, tupa, n.k. Uzuri wa umbo na sanaa za ufundi upo katika kuona. Sanaa hii hailazimishi fanani na hadhira kuwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja. c) Sanaa za maonesho Ni kazi mbalimbali za Sanaa ambazo hutegemea utendaji (mfa...
MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI FASIHI SIMULIZI: Fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutumia mazungumzo na matendo katika kuwasilisha ujumbe Fulani kwa watazamaji au wasikilizaji. Mazungumzo hayo huweza kuwa ya kuimbwa kutendwa au kuzungumzwa, Aina hii ya fasihi imepokelewa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. Msimulizi katika fasihi simulizi mbali na kutumia mdomo wake hutumia viungo vyake vya mwili kama mikono, miguu, ishara mbalimbali katika uso wake na hata kupandisha na kushusha sauti yake. Kwa ujumla anaweza kutumia mwili wake mzima katika kuwasilisha na kufanikisha ujumbe wake kwa hadhira yake ambayo huwa ana kwa ana. Isotoshe anafaulu katika kutoa picha halisi ya dhana anayotaka kuiwasilisha kama ni ya huzuni, furaha, kuchekesha n.k. Zaidi ya kusimulia, kuimba na kuigiza msanii wa fasihi simulizi huwa na nafasi ya kushirikisha hadhira yake kama wahusika katika sanaa yake. Anaweza kutimiza hayo kwa kumfanya mshiri...
MAENDELEO YA KISWAHILI ASILI YA LUGHA YA KISWAHILI Neno asili lina maana kuwa jinsi kitu au jambo lilivyotokea au lilivyoanza na tunapozungumzia asili ya lugha ya Kiswahili ina maanisha tunachunguza namna lugha hiyo ilivyoanza. Wataalamu mbalimbali wa lugha wamefanya uchunguzi juu ya asili ya lugha ya Kiswahili. Uchunguzi huo umejenga nadharia mbalimbali zinazoelezea chimbuko la lugha ya Kiswahili. Kwa ujumla historia kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili ina matatizo mengi na ndiyo maana kuna nadharia mbalimbali zinazoelezea juu ya asili ya lugha ya Kiswahili. Miongoni mwa matatizo yanayoikabili historia ya Kiswahili ni pamoja na: Hakuna uthibitisho kamili juu ya nadharia zinaelezea asili ya lugha ya Kiswahili na kuenea kwake. Uchunguzi wa asili ya Kiswahili ulifanywa na wataalamu wa kizungu ambao waliandika historia ya Kiswahili jinsi walivyoelewa wao baada ya kupata ushahidi kidogo tu. Wazawa hawakushirikishwa ipasavyo katika uchunguzi wa lugha ya Kiswahili. Hapakuwa na k...
VIAMBISHI Baadhi ya watu huchanganya dhana ya viambishi na dhana ya mofimu. Lakini ukweli ni kwamba mofimu na viambishi ni dhana mbili tofauti zenye mabwiano Fulani pia. Kwa ujumla viambishi vyote ni mofimu na mofimu zote ni viambishi SWALI: VIAMBISHI NI NINI? Viambishi ni mofimu zinazoandikwa kwenye mizizi wa neno ili kukamilisha muundo wa neno husika. Katika lugha ya Kiswahili viambishi vinaweza kuandikwa kabla ya mzizi wa neno na baada ya mzizi wa neno. kwa hiyo katika lugha ya kiswahili viambishi hutokea kabla ya mzizi wa neno na baada ya mzizi wa neno AINA ZA VIAMBISHI Lugha ya Kiswahili ina viambishi vya aina mbili VIAMBISHI AWALI/TANGULIZI Hivi ni viambishi ambavyo hutokea mwanzoni mwa mzizi wa neno na huwa ni vya aina mbalimbali A.Viambishi idadi /ngeli Viambishi hivi hupatikana mwanzoni mwa majina vivumishi kwa lengo la kuonesha idadi yaani wingi na umoja, Mfano : M – cheshi wa –zuri M – tu wa - tu Ki – ti vi-ti ...
AINA ZA SENTENSI Kuna aina kuu nne za sentensi Sentensi changamano Sentensi sahili/ huru. 3. Sentensi shurutia Sentensi Ambatano 1.SENTENSI SAHILI/HURU Hii ni aina ya sentensi ambayo hutawaliwa na kishazi huru. Kishazi hicho kinaweza kuwa kifungu tenzi kimoja ambacho kinaweza kuwa na kitenzi kikuu au kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu au kitenzi kishirikishi na shamirisho Mfano: Juma ni mzembe Juma alikuwa mzembe sana Mwalimu alikuwa nafundihsa darasani MIUNDO YA SENTENSI HURU /SAHILI Muundo wa kitenzi kikuu peke yake (tawaliwa) Mfano: Wanacheza Alinipiga Wanasoma i.Muundo wa kitenzi kikuu peke yake (tawaliwa) Mfano: Wanacheza Alinipiga Wanasoma ii.Muundo wa kitenzi na kitenzi kikuu Mfano: Alikuwa anasoma Walikuwa wanataka kufundishwa ii Muundo wa kirai na kirai kitenzi Mfano; Mwalimu anafundisha Wanafunzi wanamsikiliza iii. Muundo wa virai vite...
MATUMIZI YA SARUFI NADHARIA ZA SARUFI Dhana ya sarufi ya lugha imefafanuliwa na wataalamu mbalimbali wa sarufi. Mtaalamu James Salehe Mdee (1999) sarufi ya Kiswahili sekondari na vyuo anafafanua maana ya sarufi kuwa ni mfumo wa kanuni za lugha zinazomwezesha mzungumzaji kutunga sentensi sahihi na zenye kukubaliwa na wazawa wa lugha. Kanuni hizi hujitokeza katika lugha ya mzawa wa lugha inayohusika ambaye anaifahamu barabara lugha yake. Sarufi inajumuisha mfumo wa sauti maumbo ya maneno muundo na maana. Mtaalamu Mbundo Msokile (1992) na khamisi (1978) wanasema sarufi ni mfumo wa taratibu na kanuni zinazotawala matumizi sahihi ya matamshi, maumbo ya maneno, miundo ya tungo na maanda ya miundo ya lugha. Ni mfumo wa taratibu zinazomwezesha mzungumzaji wa lugha kutoa tungo sahihi na pia inamwezesha mtu yeyote anayezungumza kuelewa tungo zinazotolewa na mtu mwingine anayetuma lugha hiyo hiyo. F. Nkwera (1978) anasema sarufi ni utaratibu wa kanuni zinazomwezesha mzawa au mtumiaji ...
NOMINO /MAJINA (N) Majina ni aina ya maneno ambayo hutaja vitu, viumbe, hali au matendo ili kuviainisha na kuvitofautisha na vitu vingine. Mfano: Winnie, Werevu, Wema, Lulu, Mtu, Ubungo, Mungu na n.k AINA ZA MAJINA a.Majina ya kawaida Majina haya yanataja viumbe kama vile wanyama, miti, watu, ndege, wadudu. Majina yote hayo yanapoandikwa huanza kwa herufi ndogo kama yanatokea katikati ya sentensi au tungo. N:B Majina hayo sio maalumu kwa vitu Fulani tu bali kwa vitu mbalimbali. b. Majina ya Pekee. Haya ni majina maalumu kwa watu au mahali ambaye huonesha upekee kwa watu,mahali au vitu, Majina haya hujumuisha majina binafsi ya watu na majina ya mahali. Mfano: Marcus, Halima, James, Abel, Fredy, Anna Ubungo, Manzese, Tanzania, Uingereza, Africa N: B Majina hayo yanapoandikwa huanza kwa herufi kubwa C. Majina ya jamii. Haya ni majina ambayo yanataja vitu au watu wakiwa katika makundi au mafungu japo huwa majina hayo yapo katika hali ya umoja. Mfano,...
KUBAINISHA MOFIMU Kubainisha mofimu ni kuligawa neno katika mofimu zinazolijenga neno na kueleza kazi za kila mofimu ubabaishaji huo wa mofimu hufuata hatua zifuatazo 1. Kutambua aina ya neno – Yaani kama neno hilo ni tegemezi au neno changamano, Neno huru huundwa na mofimu huru na neno tegemezi huundwa na mofimu tegemezi na neno changamano huundwa na moja huru na mengine tegemezi N: B Neno huru huwa halivunjwi vunjwi kwani huundwa na mofimu huru 2. Kulitenga neno na kulivunja vunja katika mofimu zinazojenga neno hilo yaani hujenga mofimu awali, mzizi na mofimu tamati. N: B Mofimu awali, mzizi na mofimu tamati hupatikana katika maneno tegemezi na maneno changamano 3. Kueleza kazi ya kila mofimu Mfano: Bainisha mofimu katika maneno yafuatayo Hatukupendi Hili ni neno tegemezi ii. 1- Mofimu awali kianzishi, nafsi ya kwanza wingi 2 - Mofimu awali rejeshi kwa mtendwa 3 - Mofimu awali rejeshi kwa mtenda 4 - Mofimu mzizi 5 ...
UTUNGAJI Maana ya utungaji Utungaji ni pato la akili ya mtu binafsi ambayo hurejeshwa kwa fani kama vile macho, ushairi, tamthiliya au hadithi. Utungaji ni kitendo cha kuyatoa mawazo ubongoni, kuyakusanya na kisha kuyadhihirisha kwa kuyaandika au kuyazungumza. Ni kitendo cha kuunda hoja na kuyapanga katika mtiririko unaofaa katika lugha kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii husika. SIFA ZA MTUNGAJI Mtunzi analazimika kuelewa kikamilifu mada inayoshughulikiwa. Mtungaji lazima azingatie kanuni na taratibu za uandishi. Mtungaji anatakiwa kuzingatia mpango mzuri na wenye mantiki wa mawazo kutoka mwanzoni hadi mwishoni. Mtungaji anapaswa kuwa na msamiati wa kutosha ili kumwezesha kutumia lugha bora, sanifu, na fasaha. Mtunzi anapaswa kuzingatia sarufi ya lugha anayoitumia. Mtunzi anapaswa kujali nyakati zinazofaa. Mtunzi anapaswa kuwa na uwezo wa kutosha wa kuhusisha yanayoelezwa na hali halisi ilivyo katika j...